Serikali imesema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kwa kasi, yakipanda kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, sawa na ongezeko la zaidi ya mara nne ndani ya kipindi cha miaka minne.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati katika maadhimisho ya miaka 13 ya mpango wa Energising Development (EnDev), Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga, alisema mafanikio hayo yanaonyesha hatua kubwa iliyofikiwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
Alisema kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa 2024–2034, Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kwa mujibu wa Luoga, mpango wa EnDev umechangia kuwawezesha takribani watu 300,000 kupata huduma ya umeme na zaidi ya watu milioni mbili kunufaika na teknolojia za nishati safi ya kupikia.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa sehemu muhimu ya vipaumbele vya taifa kutokana na mchango wake katika kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Hata hivyo, Luoga alisema bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo uwezo mdogo wa baadhi ya kaya, hasa za vijijini, kumudu gharama za teknolojia za nishati safi pamoja na umuhimu wa kuimarisha mifumo ya udhibiti ili iendane na kasi ya ubunifu katika sekta hiyo.
Aidha, ametoa wito kwa sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika sekta ya nishati ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango wa EnDev.
“Kwa sekta binafsi, wasambazaji, wazalishaji na wajasiriamali, nawasihi kuendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na huduma kwa wateja. Mahitaji yanaongezeka na Serikali itaendelea kuwaunga mkono,” amesema Luoga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SNV Tanzania, Mary Rauscher, amesema mpango wa EnDev umechangia kuboresha upatikanaji wa nishati safi na kuinua ustawi wa jamii kwa kuwezesha familia kuokoa gharama za matumizi ya nishati.
Ameeleza kuwa wanawake na wasichana wamenufaika kwa kupata muda zaidi wa kushiriki katika elimu na shughuli za kujiongezea kipato badala ya kutumia muda mwingi kutafuta nishati za jadi za kupikia.
Rauscher alisisitiza kuwa maendeleo endelevu yanahitaji mageuzi ya mifumo katika sekta za nishati, kilimo na maji, huku akibainisha kuwa SNV itaendelea kuimarisha taasisi, kukuza masoko jumuishi na kuhakikisha wanawake, vijana na makundi yaliyotengwa wanakuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya maendeleo.





