HomeMichezoTPLB yaipiga Yanga faini milioni 100, Hersi, Ander Mtine kikaangoni

TPLB yaipiga Yanga faini milioni 100, Hersi, Ander Mtine kikaangoni

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza Klabu ya Yanga faini ya Sh milioni 100 na kuwapeleka Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine, katika Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufuatia ukiukaji wa kanuni za matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo.

Uamuzi huo ulifikiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichofanyika Julai 2, 2026, baada ya kupitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya NBC.

Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, Yanga ilikiuka Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu baada ya wachezaji na benchi la ufundi kutotumia chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo namba 233 dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, badala yake wakatumia nyumba iliyopo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara.

TPLB imeeleza kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu inayohusu vyombo vya maamuzi.

Aidha, Hersi Said na Andre Mtine wameitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya TFF kutoa maelezo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukaji unaojirudia, baada ya Yanga pia kutozwa faini ya Sh milioni 30 mwezi Mei mwaka huu kwa kosa kama hilo.

Katika maamuzi mengine, Klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kutotumia chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo dhidi ya Namungo FC uliochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Kwa upande wa KMC, klabu hiyo imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake watatu kuvaa jezi zenye namba zinazozidi 70, jambo lililokiuka kanuni za Ligi Kuu.

Wakati huo huo, TPLB imechukua hatua kali dhidi ya Stand FC Masasi baada ya kubaini udanganyifu wa usajili katika mchezo wa mchujo wa First League dhidi ya Pan African FC.

Mchezaji Ramadhani Bakari Mlaponi amefungiwa kwa miezi 12 baada ya kutumia leseni ya mchezaji mwingine, huku Stand FC ikinyang’anywa ushindi wake wa mabao 1-0 na Pan African FC kupewa ushindi wa mabao 3-0.

Pia, kocha wa Stand FC, Mbano Kizito, amefungiwa kwa miezi 12 na kutozwa faini ya Sh 500,000 kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakuwa halali kwa mujibu wa kanuni za usajili.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments