Baraza la Ulamaa la BAKWATA limeazimia kuwasimamisha Masheikh wa Mikoa mitatu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni mienendo inayokiuka misingi ya kiuongozi ya Baraza hilo.
Baraza hilo limekutana leo Julai 14, 2026 katika kikao cha dharura kilichoongozwa na Kaimu Mufti na Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ally Khamisi Ngeruko na kuazimia kuwasimamisha Masheikh hao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Said Chizenga, Masheikh waliosimamishwa ni Sheikh Walid Alhad Kawambwa wa Mkoa wa Dar es salaam, Sheikh Issa Nassor Issa wa Mkoa wa Singida pamoja na Sheikh Hassan Kiburwa wa Mkoa wa Kigoma.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa utekelezaji wa maamuzi hayo unaanza rasmi leo Julai 14, 2026.
Aidha, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Mbwana, amewateua Viongozi wa muda kushika nafasi hizo hadi pale hatua nyingine zitakapochukuliwa.
Waliopewa nafasi hizo za Ukaimu ni Sheikh Abasi Ramadhani Abasi ambaye atakuwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam, Sheikh Issa Ramadhani Simba aliyeteuliwa kuwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida na Sheikh Uwesu Mohamed Kiumbe ambaye atahudumu kama Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Kigoma.
BAKWATA pia imeielekeza Ofisi ya Katibu Mkuu kusimamia makabidhiano ya ofisi hizo ndani ya muda mfupi.




