Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Daniel Pancrasi, ameutaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuimarisha uhifadhi wa misitu, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuvutia uwekezaji katika sekta ya misitu nchini.
Pancrasi ametoa kauli hiyo alipotembelea mabanda na maeneo ya uzalishaji yanayosimamiwa na TFS katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) leo Julai 12,2026, ambapo amepongeza hatua zinazochukuliwa na wakala huo katika usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki.
Amesema matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone) katika kutambua matukio ya moto wa misitu na kufanya tathmini ya rasilimali za misitu yameongeza ufanisi wa usimamizi wa rasilimali hizo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kidijitali.
“Kwa kutumia drone na mifumo mingine ya kisasa, tunaweza kutambua rasilimali zilizopo kwa haraka, kupata taarifa kwa wakati na kufanya maamuzi sahihi zaidi katika usimamizi wa misitu,” amesema Pancrasi.


Mbali na teknolojia, ameipongeza TFS kwa namna inavyoshughulikia changamoto na malalamiko ya wananchi, huku akiitaka kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake ili waendane na mabadiliko ya mifumo ya kisasa ya utendaji kazi.
Amesema uelewa wa miongozo, taratibu na matumizi ya teknolojia miongoni mwa wahifadhi na watendaji wa ngazi mbalimbali ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa taasisi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Pancrasi amesisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji na matumizi ya mbegu bora za miti kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida zake ili kuongeza ushiriki wa jamii katika shughuli za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Pia ametaka juhudi zaidi zielekezwe katika kuendeleza zao la mianzi kwa kusambaza spishi zinazofaa katika maeneo mbalimbali kulingana na mazingira husika, akieleza kuwa hatua hiyo itachochea uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kufungua fursa zaidi za kiuchumi.
Amesema Kampuni ya Misitu ina nafasi muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya misitu, ikiwemo mianzi, na kuyawezesha kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameitaka TFS kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora na kufuatilia matumizi ya miche inayogawiwa kwa wananchi ili kuhakikisha inakua na kutoa matokeo yaliyokusudiwa, ikizingatiwa gharama zinazotumika katika uzalishaji wake.
Kwa upande wa utalii wa ikolojia, Pancrasi amewapongeza watendaji wa TFS kwa usimamizi wa vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya hifadhi za misitu na kuwataka kuongeza jitihada za kuvutia watalii wengi zaidi kupitia uhifadhi endelevu wa rasilimali za asili.
Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia, utoaji wa elimu kwa wananchi, uboreshaji wa huduma na usimamizi madhubuti wa rasilimali za misitu vitaendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya misitu na nyuki nchini.






