Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imepata tuzo mbili katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane 2026, yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma na Kanda ya Ziwa.
Katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane 2026 jijini Dodoma, COPRA imeibuka mshindi wa nafasi ya tatu katika kundi la Wakala, Mamlaka na Tume za Serikali Zinazotoa Huduma na Uzalishaji.
Aidha, Nanenane Kanda ya Ziwa, COPRA imepata nafasi ya tatu katika kundi la Taasisi za Usimamizi na Udhibiti, miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika kundi hilo.
Mafanikio haya yanaakisi juhudi za COPRA katika kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu, huduma na taarifa kwa wadau, pamoja na kuimarisha uelewa kuhusu uzalishaji, ubora, biashara na masoko ya nafaka na mazao mchanganyiko.
Katika siku nane za maonesho, COPRA iliendesha shughuli mbalimbali, zikiwemo semina kuhusu Kanuni za Usimamizi wa Zao la Parachichi, Kanuni za Kilimo cha Mkataba na Kanuni za Udhibiti wa Ubora na Viwango.
Kupitia Siku ya Kakao, wadau walijadili fursa za masoko ya ndani, uongezaji thamani na nafasi ya vijana katika biashara ya kakao, ikiwemo utengenezaji wa chokoleti, siagi ya kakao na vipodozi.
COPRA pia iliendesha Agribusiness Influencers Day, ambapo watayarishaji wa maudhui walikutana na viongozi na wataalamu wa COPRA na kujengewa uelewa kuhusu uzalishaji, kanuni, urasimishaji wa biashara, mifumo ya masoko na COPRA MIS, kwa lengo la kuwawezesha kusimulia sekta kwa usahihi.
Aidha, wadau walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu matumizi na uongezaji thamani wa mazao ya jamii ya mikunde kupitia shughuli za kuonja vyakula na mapishi mbalimbali.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, COPRA pia ilikutana na viongozi na wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo viongozi kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, katika majadiliano kuhusu biashara ya mazao, masoko ya kikanda na mifumo ya kidijitali.
Mafanikio haya yanaipa COPRA hamasa ya kuendelea kuboresha huduma, kuimarisha masoko, kurasimisha biashara na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050.”




