Mradi wa kisasa wa uchakataji wa majitaka unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) eneo la Mbezi Beach, umefikia asilimia 88 ya utekelezaji na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya kaya 11,000 katika Wilaya ya Kinondoni.
Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 124 unatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kisasa ya majitaka na usafi wa mazingira katika Afrika Mashariki.




Kwa mujibu wa DAWASA, mradi huo unahusisha ulazaji wa mtandao wa mabomba ya majitaka wenye urefu wa kilomita 101, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma majitaka, chemba zaidi ya 2,300 pamoja na mtambo wa kisasa wa kuchakata majitaka.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu na utanufaisha wakazi wa kata nne za Kinondoni ambazo ni Kawe, Kunduchi, Mbezi Juu na Wazo.
Mbali na kuboresha huduma ya majitaka na usafi wa mazingira, mradi huo unatarajiwa kuwezesha uzalishaji wa bidhaa nyingine muhimu kutokana na uchakataji wa majitaka, ikiwamo mbolea na gesi.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za majitaka kwa wakazi wa maeneo hayo na kuchangia katika kuboresha afya ya jamii pamoja na mazingira.







