
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaonya wafanyabiashara na walipakodi wanaojihusisha na matumizi mabaya ya mifumo ya kielektroniki ya kodi, ikisema itaendelea kuwafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaotumia mbinu hizo kuikosesha Serikali mapato.
Onyo hilo limekuja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kumhukumu mfanyabiashara Frank Kagale kifungo cha miaka 20 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa yanayohusisha kukwepa kodi, kuisababishia Serikali hasara na kudanganya mifumo ya kielektroniki.




Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 11, 2026 jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na mawasiliano TRA, CPA. Paul Walalaze amesema Kagale alikuwa akijihusisha na uuzaji wa risiti za EFD kwa wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, ambapo risiti hizo zilitumika katika madai ya marejesho ya kodi.
CPA. Walalaze amesema TRA haitashughulikia mtu mmoja aliyebainika katika vitendo hivyo, bali inaendelea kuwafuatilia wote waliohusika katika mnyororo mzima kwa lengo la kubaini wahusika, kukusanya kodi iliyokwepwa pamoja na adhabu zake.

TRA imeeleza kuwa vitendo hivyo vina madhara makubwa kwa Taifa kwa sababu vinapunguza mapato ambayo yangetumika kugharamia sekta muhimu kama elimu, afya, maji, miundombinu, nishati na usalama, hivyo ukwepaji kodi unapunguza uwezo wa Serikali kutekeleza mahitaji hayo kwa wananchi.
Vile vile amesema TRA itaendelea kutumia mifumo ya kiteknolojia, uchambuzi wa taarifa, ukaguzi na upelelezi, sambamba na kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali, ili kubaini na kuchukua hatua dhidi ya watu au mitandao inayojihusisha na udanganyifu wa mifumo ya kodi.
Katika hatua nyingine, TRA imewataka wananchi kushiriki katika kulinda mapato ya Taifa kwa kudai risiti halali kila wanapofanya manunuzi, kukataa kushiriki katika mipango ya kukwepa kodi na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyoweza kuhujumu mapato ya Serikali.





