Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe Joseph Butiku amesema Tanzania inahitaji kwanza kupata ukweli kuhusu vurugu zilizotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kabla ya nchi kuweza kumaliza mvutano unaoendelea kuhusu matukio hayo.
Mzee Butiku, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, amesema tume mpya ya uchunguzi inapaswa kupewa nafasi ya kufanya kazi na kubaini kilichotokea pamoja na nani alikuwa nyuma ya vurugu hizo.
“Vurugu hii nani alikuwa nyuma yake? Ni jambo muhimu sana kugfahamu hilo, bila tume unajuaje? Rais anajuaje? Mimi na wewe tunajuaje?” amesema.
Amesema tume hiyo inatoa fursa kwa Watanzania kutafuta na kutafakari yaliyotokea, huku ikimsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kupata ushauri kabla ya kufanya maamuzi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Mzee Butiku amesema wananchi hawapaswi kutumia muda mwingi kuijadili tume hiyo kabla haijafanya kazi, akisisitiza umuhimu wa kusubiri matokeo ya uchunguzi.
“Mimi bado nashauri kama nilivyoshauri ile tume ya kwanza tuikubali. Ameshafanya, tuache maneno mengi, ifanye kazi, tuje tuone matokeo ya kazi yake ndipo tuseme,” amesema.
Amesema Rais hawezi kujua kila kitu kilichotokea wakati wa vurugu hizo, akisema ni muhimu kuwepo kwa mchakato unaoweza kukusanya taarifa kutoka kwa watu mbalimbali na kusaidia kuonyesha kilichotokea.
Kwa mujibu wa Mzee Butiku, taarifa zitakazopatikana zinaweza kusaidia taifa kuwa na uelewa wa pamoja badala ya kuendelea kutegemea mitazamo inayokinzana kuhusu matukio ya Oktoba.
Amesema ukweli huo unaweza pia kumsaidia Rais kupata ushauri utakaowezesha taifa kufikia uamuzi kuhusu namna ya kukabiliana na matokeo ya vurugu hizo.
Hata hivyo, Mzee Butiku amesema mchakato huo unahitaji pia Watanzania kuanza kuaminiana na kuvumiliana, kwa kuwa changamoto ya kitaifa hayawezi kutatuliwa ikiwa kila upande utamwona mwingine kama mpinzani wa kila jambo.
“Demokrasia ni imani. Msipoaminiana haitakuwepo hata siku moja,” amesema.
Ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kusikilizana na kujibu hoja kwa hoja badala ya kupingana katika kila jambo.
“Tusipingane kila kitu, tuanze kuongozana kwa hoja,” amesema.
Mzee Butiku amesema ukweli utakaopatikana kupitia tume unaweza kusaidia Tanzania kuamua namna ya kwenda mbele na kurejesha uaminifu miongoni mwa wananchi.
Kwa mtazamo wake, kupata majibu kuhusu kilichotokea na nani alikuwa nyuma ya vurugu ni hatua muhimu katika kusaidia Tanzania kuondokana na mvutano wa kisiasa unaoendelea kuhusu uchaguzi huo.




