HomeHabariRC Chalamila atoa onyo kali kwa mabasi yanayokiuka agizo lake

RC Chalamila atoa onyo kali kwa mabasi yanayokiuka agizo lake

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa onyo kali kwa wamiliki na madereva wa mabasi wanaokaidi agizo la Serikali la kuanzia safari katika Kituo cha Mabasi Magufuli na badala yake kutumia vituo visivyo rasmi katika eneo la Shekilango.

Chalamila ametoa onyo hilo leo wakati akikagua utekelezaji wa agizo la kufungwa kwa vituo visivyo rasmi katika eneo hilo, akisisitiza kuwa hataki kuona basi likipakia au kushusha abiria Shekilango.

“Sitaki kuona basi eneo la Shekilango. Yeyote atakayekaidi nitamfikisha mahakamani,” amesema Chalamila.

Amesema mmiliki au dereva atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani, akisisitiza kuwa Serikali haitaruhusu shughuli za usafirishaji wa mabasi kufanyika kiholela.

Chalamila amesema endapo kutakuwa na changamoto au mapungufu katika Kituo cha Mabasi Magufuli, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na kuboresha huduma, hivyo hakuna sababu ya wadau kutumia maeneo yasiyo rasmi.

Amesema wamiliki wanaotaka kuwa na vituo binafsi wanaweza kuomba maeneo ndani ya kituo hicho na kuyatumia kwa kufuata taratibu zilizowekwa, badala ya kuanzisha vituo kiholela.

Aidha, amewaagiza wamiliki na abiria kuhakikisha wanakitunza kituo hicho ili kiendelee kuwa katika hali nzuri na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amewaonya viongozi watakaopokea fedha kutoka kwa wafanyabiashara au watu wenye uwezo wa kifedha ili kuruhusu mabasi kuendelea kupaki nje ya kituo hicho, akisema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Pia amewaonya madereva na wamiliki wa mabasi wanaopanga kugoma kutokana na agizo hilo kuacha mara moja, akisisitiza kuwa Serikali haitakubali vitendo vinavyolenga kukwamisha utekelezaji wa utaratibu huo.

Chalamila amesema Serikali itawachunguza wamiliki wa mabasi wanaokaidi agizo hilo ili kubaini sababu zinazowafanya kukataa kutumia kituo hicho, ikiwemo uwezekano wa kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya au watu kwa njia zisizo halali.

Ametoa maagizo kwa Meneja wa Kituo cha Mabasi Magufuli kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo hayo, huku akiiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuchukua hatua dhidi ya mabasi yanayokiuka taratibu, ikiwemo kufuta leseni pale inapobainika kuwa kuna ukiukwaji wa sheria.

Katika ziara hiyo, Chalamila pia amemsamehe Mkurugenzi wa kampuni ya mabasi ya Tilisho, aliyekuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuendelea kukiuka agizo la kupaki nje ya  kiholela.

Amesema Kituo cha Mabasi Magufuli kinasimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na kwamba Serikali haitarajii kuwepo kwa vituo vingine visivyo rasmi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wakati wa ziara hiyo, kabla ya agizo la Serikali, kituoni hapo yalikuwa yakiingia mabasi takribani 150 kwa siku. Baada ya utekelezaji wa agizo hilo, idadi imeongezeka hadi mabasi 360 kwa siku.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amesema hakuna utaratibu unaoruhusu abiria kushushwa nje ya kituo hicho, akisisitiza kuwa mabasi yote yanapaswa kutumia miundombinu rasmi iliyowekwa.

Msando amesema magari pia yanapaswa kufuata taratibu za ukaguzi zilizowekwa na vyombo vya dola na kupiga marufuku matumizi ya hifadhi za barabara zisizo rasmi kwa ajili ya kupakia au kushusha abiria, akisema hali hiyo inachochea foleni na kuhatarisha usalama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kibamba, Angela Kairuki, amesema Kituo cha Mabasi Magufuli kimeweza kutoa ajira kwa zaidi ya watu 2,000 na kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

Baadhi ya wafanyabiashara katika kituo hicho wamepongeza hatua ya Serikali kurejesha shughuli zote za mabasi kituoni hapo, huku wakiomba Serikali kuboresha baadhi ya huduma, ikiwemo matengenezo ya lifti na mageti.

Wadau hao wamesema maboresho ya miundombinu yataongeza ufanisi wa kituo hicho na kuwapa abiria pamoja na wafanyabiashara mazingira bora ya kupata huduma.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments