HomeBiasharaTawi jipya CRDB Tinde: Akaunti 14,000 zafunguliwa

Tawi jipya CRDB Tinde: Akaunti 14,000 zafunguliwa

SHINYANGA — Matumizi ya huduma rasmi za kifedha miongoni mwa wananchi wa Tinde, mkoani Shinyanga, yameongezeka katika miaka ya karibuni, hali inayodhihirisha kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha katika eneo hilo.

Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde, ambapo imeelezwa kuwa zaidi ya akaunti 14,000 zimefunguliwa kupitia tawi hilo, ikionyesha kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kibenki miongoni mwa wananchi.

Uzinduzi wa tawi hilo umefanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, huku CRDB ikieleza kuwa uwekezaji huo umetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kifedha na umuhimu wa kuzisogeza karibu na wananchi.

Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Exavery Makwi, amesema ongezeko hilo limewezesha kupanuka kwa huduma za kifedha, ikiwemo mikopo kwa wafanyabiashara, wakulima, watumishi pamoja na vikundi vya vijana na wanawake, kwa lengo la kuwawezesha kupata mitaji na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Makwi amesema uwekezaji wa tawi hilo umegharimu Shilingi milioni 650, zilizotumika katika ununuzi wa ardhi, ujenzi wa jengo na uwekaji wa vifaa.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutoa huduma za kibenki, CRDB Tinde imechangia maendeleo ya jamii kupitia sekta ya elimu kwa kutoa madawati, vifaa vya ofisi na vifaa vya michezo, pamoja na kushiriki katika ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Tinde.

Aidha, uwepo wa tawi hilo umechangia upatikanaji wa ajira za kudumu na za muda, huku mikopo yenye riba nafuu na mikopo isiyokuwa na riba ikitolewa kwa watumishi, wafanyabiashara, wakulima na vikundi vya vijana na wanawake.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments