Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Palamagamba Kabudi, amezitaka nchi za Afrika kutumia kikamilifu mifumo ya kikanda na kibara ya ulinzi na amani katika kuzuia na kutatua migogoro na kudumisha utulivu barani humo.
Kabudi ameyasema hayo Agosti 30, 2026, jijini Luanda, Angola, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliojadili mifumo ya kuzuia na kutatua migogoro barani Afrika.
Akihutubia mkutano huo kwa niaba ya Rais Samia, Kabudi amesema mafanikio katika utatuzi wa migogoro yanategemea kuheshimiwa na kutekelezwa kwa sheria, taratibu na mikataba iliyowekwa na nchi wanachama kupitia taasisi za kikanda.

“Tunahitaji kuendelea kuweka msisitizo kupitia maamuzi yetu ya pamoja ili kuzuia migogoro na kuhakikisha tunapata matokeo chanya na ya kudumu. Tanzania inaunga mkono kikamilifu jitihada zote zinazolenga kuimarisha ulinzi, amani na usalama barani Afrika,” amesema.
Amesema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano na kutumia vyombo vilivyopo katika ngazi za kikanda na kibara ili kushughulikia migogoro kwa njia za amani na kupata suluhisho endelevu.
Tanzania imeendelea kushiriki katika juhudi za kidiplomasia za kuzuia na kutatua migogoro pamoja na kuimarisha amani na usalama barani Afrika, msimamo unaoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.





