Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji Kigamboni, ikisema uzalishaji wa maji unaofanywa na mradi huo unatosheleza mahitaji ya sasa ya wakazi wa eneo hilo.
Kamati hiyo ilitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo na kujionea uwezo wake wa kuzalisha na kuhudumia wananchi wa Kigamboni na maeneo ya jirani.
Mradi huo kwa sasa unazalisha lita milioni 37 za maji kwa siku, wakati mahitaji ya sasa ya wakazi wa Kigamboni yanafikia takribani lita milioni saba kwa siku.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema utekelezaji wa mradi huo umekamilika na tayari wananchi wameanza kunufaika na huduma ya maji.
Alisema kwa sasa Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na kazi ya kusambaza maji, kufanya maunganisho ya wateja pamoja na kupanua mtandao ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wa Kigamboni na maeneo ya jirani.




Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga, aliwahakikishia wakazi wa Kigamboni kuwa uzalishaji wa maji kupitia mradi huo unatosheleza mahitaji ya sasa ya eneo hilo.
Kiswaga aliwataka wananchi ambao bado hawajaunganishwa na huduma hiyo kutumia fursa iliyopo kwa kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa maji ili wanufaike na miundombinu iliyowekwa na Serikali.
“Baada ya kuona utekelezaji, sasa ni muhimu kuwaambia wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa huduma ya maji ili waweze kunufaika na miundombinu iliyowekwa. Tayari DAWASA wametueleza kuwa kuna ofa ya kuunganishiwa kwa punguzo, hivyo ni wakati wa kuchangamkia fursa,” amesema Kiswaga.
Aidha, Kiswaga ameitaka DAWASA kuendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha huduma ya maji inawafikia walengwa wengi zaidi, akisema uwezo mkubwa wa uzalishaji uliopo unatoa fursa ya kuongeza kwa kasi idadi ya wananchi wanaounganishwa na huduma hiyo.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia mradi huo unaleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi wa Kigamboni.





