Friday, November 14, 2025
spot_img
HomeHabariBridge of Hope ya Ujerumani yarejesha tabasamu Dongobesh

Bridge of Hope ya Ujerumani yarejesha tabasamu Dongobesh

Na Mwandishi Wetu, MANYARA

Taasisi ya Bridge of Hope kutoka Ujerumani imewarejeshea tabasamu wanafunzi zaidi ya 2,000 wa Dongobesh, Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, baada ya kuchimba kisima kirefu cha maji safi kilicholenga kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.

Wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lea pamoja na Shule ya Sekondari Dongobesh walikuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji wakati wa masomo, huku wakazi wa vijiji jirani wakilazimika kutumia maji machafu kwa matumizi ya nyumbani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana wilayani Mbulu, Mwanzilishi wa Bridge of Hope, Arnd Weil, alisema kisima hicho kirefu kilichogharimu Sh milioni 100 kimelenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya maji safi kwa wanafunzi na wakazi wa Dongobesh.

“Tumeamua kusaidia jamii hii kwa sababu tuliona jinsi changamoto ya maji inavyoathiri masomo na afya ya wanafunzi. Tunataka kuona watoto wanajikita katika elimu badala ya kutumia muda kutafuta maji,” alisema Weil.

Ameongeza kuwa wanafunzi na wananchi wa eneo hilo tayari wameanza kunufaika na huduma ya maji safi, hatua itakayowarahisishia shughuli za kila siku na kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni.

“Mradi huu umeelekezwa zaidi kwa Shule ya Msingi na Sekondari Dongobesh baada ya kubaini kuwa wengi wao walikuwa wanapata matatizo ya kiafya kutokana na kutumia maji yasiyo salama,” aliongeza.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Simendu, aliipongeza taasisi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii, akisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kutatua changamoto za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.

“Serikali inatambua mchango wa taasisi kama Bridge of Hope. Ushirikiano wa aina hii unasaidia kuongeza tija kwa jamii na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali,” alisema Simendu.

Kwa upande wake, Mwanzilishi Mwenza wa taasisi hiyo, Simone Weil, alisema waliguswa na hali ya wanafunzi wa Shule ya Lea waliokuwa wakikosa maji safi, jambo lililowasukuma kutoa ufadhili wa kuchimba kisima hicho.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Anna Paul, alieleza furaha yao baada ya kupata huduma ya maji safi shuleni, akisema hatua hiyo imeleta ahueni kubwa hasa kwa wasichana waliokuwa wakikumbana na changamoto wakati wa hedhi.

“Tunashukuru kwa msaada huu. Zamani tulikuwa tunapoteza muda na wakati mwingine tunashindwa kuhudhuria masomo, lakini sasa tunapata maji muda wote,” alisema Anna.

Mradi huo unatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa hali ya maisha ya wanafunzi na jamii ya Dongobesh, sambamba na kuchochea maendeleo ya elimu na afya.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments