Wananchi wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameipokea kwa hamasa kampeni ya “Tunatiki”, inayolenga kuhamasisha uungwaji mkono kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amefanya ziara mkoani humo akiwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na kumuamini Dk. Samia katika uongozi wake.
Akizungumza na wananchi wa Bukoba, Nyalandu amesema Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono Rais Samia kutokana na juhudi zake katika kuleta maendeleo na kuimarisha umoja wa kitaifa.
“Tuendelee kumuamini Rais wetu Dk. Samia, tumpe kura za kutosha ifikapo Oktoba 29 ili aendelee kutupeleka kwenye maendeleo zaidi,” amesema Nyalandu.
Ziara hiyo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya “Tunatiki”, ambayo inahusisha viongozi mbalimbali wa chama na serikali, ikilenga kuhamasisha mshikamano na uungwaji mkono kwa Rais Samia katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.






