Tuesday, April 21, 2026
spot_img
HomeBiasharaKampuni ya Saturn Corporation Yalenga Viwango vya Kimataifa Kupitia ISO

Kampuni ya Saturn Corporation Yalenga Viwango vya Kimataifa Kupitia ISO

Saturn Corporation Limited, kampuni ya uunganishaji wa magari yenye makao yake Kigamboni, Dar es Salaam, inaongoza juhudi za kuelekea kupata uthibitisho wa viwango vya kimataifa vya ISO, hatua inayokuja muda mfupi baada ya kuanzisha kiwanda chake cha kuunganisha malori aina ya HOWO, na kuiweka miongoni mwa kampuni changa zinazojipanga kuendana na viwango vya uzalishaji vya kimataifa.

‎Kampuni hiyo inasema hatua hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya ndani kadri inavyoendelea kupanua shughuli zake, pamoja na kuongeza imani kwa magari yanayounganishwa hapa nchini.

‎ Afisa Mkuu wa Uendeshaji,  Mehul Sachdev, anasema uamuzi huo ni wa kimkakati na wa kuangali mbele 
‎“Kuanzia mwanzo, tuliweka kipaumbele katika kujenga mifumo imara na rasilimali watu yenye ujuzi inayoweza kufikia viwango vya kimataifa vya uzalishaji.

‎ Uthibitisho wa ISO ni mwendelezo wa mkakati huo. Unatuwezesha kuweka mifumo yetu katika mpangilio rasmi na kuhakikisha tunadumisha ubora tunapokua,” anasema Mehul
‎Kwa kushirikiana na kampuni ya Sinotruk, Saturn imejenga kiwanda kinachosaidia sekta muhimu za uchumi ikiwemo ujenzi, madini, usafirishaji na kilimo. Kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya Watanzania 330 wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali kama uhandisi, uunganishaji, udhibiti wa ubora na utawala. Mafunzo yanaanza tangu hatua ya ajira, yakilenga kuwajengea wafanyakazi ujuzi wa vitendo, nidhamu ya kazi pamoja na usalama na umakini unaohitajika katika uzalishaji wa kisasa.

Kampuni inaendelea na mchakato wa kupata uthibitisho wa ISO 9001, ISO 14001 na ISO 45001, ambao unatarajiwa kuimarisha zaidi mifumo ya ndani kwa kuweka udhibiti madhubuti katika ubora, usimamizi wa mazingira na afya na usalama kazini. Kwa vitendo, hatua hii ina maana ya kupunguza makosa katika uzalishaji, kuboresha ufuatiliaji wa mchakato mzima wa uzalishaji, kupunguza hatari za uendeshaji na kuhakikisha mazingira salama zaidi ya kazi.

‎“Kwa upande wa biashara, pia tunajiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kukidhi matakwa ya kisheria, kuvutia wateja wakubwa wa taasisi na kushiriki katika minyororo ya thamani ya kikanda na kimataifa ambako uthibitisho wa viwango ni hitaji la msingi,” anaongeza Mehul.

‎Kwa kampuni inayojihusisha na uunganishaji wa magari mazito, uthibitisho huu unalenga kuhakikisha uzalishaji unaokuwa na utabirika zaidi, kuimarisha ubora wa bidhaa zinazotoka kiwandani na kujenga uaminifu wa chapa katika soko. Pia unaiwezesha Saturn kuondoka katika mfumo wa kawaida wa uunganishaji na kuelekea kwenye uzalishaji unaoongozwa na viwango, unaoweza kuhimili ukuaji bila kupunguza ubora.

‎Saturn pia inashirikiana na taasisi za serikali kuwajumuisha wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi (TVET) katika shughuli zake kupitia programu za mafunzo kwa vitendo. Mpango huu unalenga kuziba pengo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya viwandani, huku ukichangia kukuza rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika.

‎“Tunaendelea pia kupanua uwezo wetu wa uzalishaji ili kujumuisha aina mbalimbali za magari kuanzia magari madogo ya kibiashara hadi malori makubwa, na hili linahitaji nidhamu kubwa katika uendeshaji,” anaongeza.

‎Kampuni inalenga kufikia uzalishaji wa jumla ya magari 10,000 ifikapo mwaka 2027, kiwango ambacho kinahitaji uthabiti katika kila hatua ya uzalishaji. Uthibitisho wa ISO unatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika kusaidia upanuzi huo na kuhakikisha ukuaji unaendelea kwa misingi imara.

‎“Kuwa na mifumo inayotambulika kimataifa kunatusaidia kusimamia ukuaji huo bila kuathiri ubora, usalama na uwajibikaji wa kimazingira,” anasema.

‎Nje ya kiwanda, ukuaji wa Saturn tayari unaanza kuonekana katika mnyororo mpana wa thamani. Wasafirishaji, wauzaji wa vipuri, mafundi na watoa huduma wengine wanazidi kunufaika na uwepo wa magari yanayounganishwa hapa nchini.

‎ Kadri kampuni inavyoimarisha mifumo yake, inatarajiwa pia kuongeza viwango vya utendaji katika sekta hizi zinazohusiana.

‎“Tunajenga mfumo wa uzalishaji unaoweza kushindana hata nje ya soko la ndani,” anahitimisha.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments