Sunday, November 9, 2025
spot_img
HomeHabariMbibo aongoza kikao cha wataalam kujadili utoroshaji madini nchini

Mbibo aongoza kikao cha wataalam kujadili utoroshaji madini nchini

✍🏿Asema ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda rasilimali za taifa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, ameongoza kikao cha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kujadili mikakati ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.

Kikao hicho kimefanyika Oktoba 7, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Madini, Mtumba jijini Dodoma, kikilenga kuweka mikakati shirikishi ya kulinda rasilimali za taifa dhidi ya vitendo vya utoroshaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mbibo alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za taifa, hasa madini, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Utoroshaji wa madini ni tishio kwa uchumi na usalama wa taifa letu. Tunapaswa kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti mianya yote inayochangia vitendo hivi,” alisema Mbibo.

Aliongeza kuwa utoroshaji wa madini umekuwa ukisababisha upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali, na hivyo ipo haja ya kuchukua hatua za dharura kwa kuunganisha nguvu za pamoja katika kudhibiti vitendo hivyo haramu.

“Madini ni miongoni mwa rasilimali muhimu zinazochochea maendeleo ya taifa letu. Hatuwezi kukubali kuendelea kupoteza mapato kwa sababu ya mianya ya utoroshaji. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kama wazalendo kushiriki katika vita hii,” alisisitiza.

Mbibo alieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa udhibiti wa madini kuanzia migodini, vituo vya ukaguzi, viwanja vya ndege, bandari na mipaka yote ya nchi, ili kuhakikisha ufuatiliaji unafanyika kwa ufanisi.

Aidha, alipendekeza kuundwa kwa timu maalum za kitaifa zenye wataalam kutoka taasisi mbalimbali zitakazoshirikiana katika kufanya uchunguzi, ufuatiliaji na ulinzi wa madini, hasa katika maeneo yenye mianya mikubwa ya utoroshaji.

“Tunapaswa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya kuchunguza na kubaini madini, hususan madini ya vito, ili kusaidia kubaini mbinu mpya zinazotumiwa na wanaojihusisha na utoroshaji,” alisema.

Mbibo pia alipendekeza kuanzishwa kwa mpango wa mafunzo endelevu kwa wataalam wanaofanya kazi katika maeneo ya ukaguzi ili kuwajengea uwezo wa kutambua aina mbalimbali za madini, mbinu za usafirishaji haramu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kudhibiti biashara hiyo.

Katika hitimisho la kikao hicho, wadau walikubaliana kuweka mikakati ya haraka ya utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa, ikiwemo kuandaa mpango kazi wa pamoja utakaohakikisha udhibiti wa utoroshaji wa madini unafanyika kwa ufanisi na kwa muda mrefu.

Kikao hicho kilihusisha ushiriki wa taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments