Waajiri katika sekta ya umma wamekumbushwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha michango ya watumishi kwa wakati katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ili kuhakikisha wanachama wanapata mafao na stahiki zao kwa wakati wanapostaafu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF, Hilda Mkunna, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.
Mkunna alisema pamoja na waajiri kutimiza wajibu wao wa kuwasilisha michango kwa wakati, watumishi pia wanapaswa kuwa na utamaduni wa kufuatilia taarifa za michango yao mara kwa mara ili kujiridhisha kuwa michango yao inawasilishwa kwa usahihi.
Alisema hatua hiyo itasaidia kubaini mapema changamoto zozote zinazoweza kujitokeza na kuhakikisha wanachama hawapati usumbufu wanapofikia umri wa kustaafu.




Akizungumzia kampeni ya “Tunalipa Jana”, Mkunna alisema inalenga kuhakikisha mwanachama anayewasilisha nyaraka zote muhimu kwa ukamilifu analipwa mafao yake mara tu anapostaafu, bila kuchelewa.
Aliongeza kuwa maendeleo ya teknolojia yameiwezesha PSSSF kuboresha utoaji wa huduma, ambapo wanachama sasa wanaweza kupata huduma nyingi kupitia mifumo ya kidijitali bila kulazimika kufika ofisini.
“Mwanachama anaweza kufuatilia taarifa zake kupitia programu ya PSSSF Kiganjani, kutumia PSSSF Member Portal, au kutembelea ofisi zetu zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanachama wa PSSSF, Profesa Herbert Qambalo, aliipongeza PSSSF kwa kuendelea kutumia teknolojia katika utoaji wa huduma.
“Nimefurahishwa na matumizi ya mifumo ya kidijitali. Kupitia mfumo huu nimeweza kuona historia ya michango yangu tangu nilipoajiriwa, kiwango kinachochangwa na mwajiri pamoja na mchango wangu binafsi. Hii inaongeza uwazi na kuimarisha imani ya wanachama kwa Mfuko,” alisema Prof. Qambalo.
Naye Mwalimu Maombi Kyando kutoka Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, alisema huduma za kidijitali za PSSSF zimerahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma mbalimbali, hatua inayowawezesha wanachama kufuatilia michango yao kwa urahisi zaidi.





