Saturday, November 8, 2025
spot_img
HomeAfyaUtafiti: Zaidi ya 70% ya Watanzania wana tatizo la meno

Utafiti: Zaidi ya 70% ya Watanzania wana tatizo la meno

DAR ES SALAAMDk. Baraka Nzobo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno katika Wizara ya Afya, amesema zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanakabiliwa na matatizo ya meno na fizi, huku changamoto kubwa ikiwa ni uhaba wa wataalamu wa meno, kwani nchi inahitaji zaidi ya madaktari bingwa 300, lakini waliopo hawazidi 100.

Kauli yake ilitolewa wakati wa Kongamano la 15 la Afya ya Kinywa na Meno, lililofanyika jijini Dar es Salaam, ambalo limewaleta pamoja wataalamu wa afya ya kinywa, watafiti, watunga sera na wadau wa sekta ya afya kujadili matokeo ya utafiti na njia bora za kuboresha huduma za meno nchini.

Dk. Nzobo alisema utafiti huo unaonyesha changamoto kubwa za kiafya zinazokabili watoto na watu wazima, zikihusisha kuoza meno, mpangilio usio sahihi wa meno na ugonjwa wa fizi, huku akisisitiza kuwa elimu kwa jamii na tabia bora za kiafya ni suluhisho la msingi.

Kongamano hilo pia limeangazia uhitaji wa huduma za kinywa kuingizwa kikamilifu katika Bima ya Afya kwa Wote (UHC), ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila vikwazo vya gharama. Dk. Nzobo alihimiza mashirikiano ya karibu kati ya taasisi za elimu, sekta binafsi na serikali ili kufanikisha huduma bora na upatikanaji wa wataalamu zaidi.

Prof. Emmanuel Balandya, Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, alisema kongamano hilo linaonyesha juhudi za chuo kuhakikisha elimu ya afya ya kinywa inakuwa endelevu na inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku akisisitiza uhitaji wa ubunifu na ujuzi wa kidijitali kwa wataalamu wa meno.

Kongamano limeibua mjadala muhimu kuhusu juhudi za kitaifa za kupunguza matatizo ya meno, likisisitiza kuwa elimu, upatikanaji wa huduma, na matibabu ndani ya mfumo wa UHC ni nguzo za kuhakikisha Watanzania wote wanapata afya bora na tabasamu endelevu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments