Msemaji wa Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, amesema wanafunzi 130 wa shule ya Kikatoliki waliokuwa bado wanashikiliwa na watekaji nyara wameachiwa huru, kufuatia uvamizi uliotokea mwezi Novemba mwaka huu katika Jimbo la Niger.
Taarifa hiyo ilitolewa na msemaji wa Rais, Onanuga Bayo, kupitia chapisho kwenye mtandao wa X jana Jumapili, Desemba 21, 2025. Alisema kuwa watoto hao wanatarajiwa kufika mjini Minna leo Jumatatu na kuungana na wazazi wao kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi.
Wanafunzi hao ni miongoni mwa zaidi ya wanafunzi 300 pamoja na wafanyakazi 12 waliotekwa nyara na watu wenye silaha kutoka shule ya bweni ya St. Mary’s Catholic iliyopo katika kijiji cha Papiri, Jimbo la Niger.

Hapo awali, Chama cha Wakristo cha Nigeria kilieleza kuwa wanafunzi 50 waliweza kutoroka wakati wa tukio hilo, huku Serikali ya Nigeria ikitangaza Desemba 8 kuwa imefanikiwa kuwaokoa wanafunzi 100.
Kwa mujibu wa Onanuga, jumla ya wanafunzi walioachiwa huru hadi sasa imefikia 230, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa katika juhudi za Serikali ya Nigeria kukabiliana na matukio ya utekaji nyara nchini humo.




