HomeAfyaCRDB, CCBRT kushirikiana kuimarisha huduma jumuishi kwa watu wenye mahitaji maalum

CRDB, CCBRT kushirikiana kuimarisha huduma jumuishi kwa watu wenye mahitaji maalum

Katika jitihada za kuongeza ujumuishi wa wananchi katika huduma za kifedha nchini, Benki ya CRDB imeingia makubaliano ya ushirikiano na taasisi ya CCBRT kwa lengo la kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili kutambua mahitaji na kuwahudumia kwa ufanisi watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo tayari imeanza kuwafundisha wafanyakazi wake lugha ya alama ili kurahisisha mawasiliano na huduma kwa wateja wenye changamoto za kusikia.

Amesema hadi sasa wafanyakazi 90 tayari wamepata mafunzo hayo, sambamba na hatua nyingine za kuboresha miundombinu ya matawi ya benki ili yawe rafiki kwa makundi yote ya wateja.

Dkt. Nsekela ametaja maboresho hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia za kupitishia viti vya magurudumu (walking ramps), uwekaji wa alama na mabango ya maelekezo yaliyo wazi, uboreshaji wa vyoo kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum, pamoja na ATM zenye huduma ya sauti kwa kusaidia wateja wenye changamoto za kuona.

Aidha, amesema katika matukio muhimu ya benki hiyo, ikiwemo Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanahisa, hutumika mfasiri wa lugha ya alama ili kuhakikisha ushirikishwaji mpana.

Ameongeza kuwa CRDB inaendelea kubuni huduma jumuishi za kifedha zikiwemo SimBanking, huduma za wakala, benki mtandao, ATM na huduma za mauzo (POS), pamoja na matawi ya benki yanayotembea ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Ushirikiano wetu na CCBRT unalenga kukuza ubunifu huu ili kuwafikia watu wengi zaidi, hasa makundi yaliyosahaulika lakini yenye mchango muhimu katika uchumi wetu,” amesema Dkt. Nsekela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brenda Msangi, amesema huduma za kifedha ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya umasikini na zinapaswa kumfikia kila mwananchi bila ubaguzi.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kujenga wataalamu wenye uwezo wa kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum, pamoja na kuboresha miundombinu ya taasisi za kifedha ili ziwe rafiki kwa wote.

“Maisha bora kwa kila mtu hayawezi kufikiwa kama huduma za kifedha zinawafikia watu wachache tu. Ushirikiano huu utasaidia kuhakikisha kundi hili muhimu linajumuishwa kikamilifu kiuchumi,” amesema Msangi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments