HomeHabariTanzania, Ujerumani wakubaliana blioni 60.7/- kuboresha huduma za maji  Tunduma, Vwawa-Mlowo

Tanzania, Ujerumani wakubaliana blioni 60.7/- kuboresha huduma za maji  Tunduma, Vwawa-Mlowo

Serikali imesaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 20 (sawa na shilingi bilioni 60.7) kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), kwa ajili ya kufadhili mradi wa uboreshaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square jijini Dodoma, ambapo Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba, huku upande wa Ujerumani ukiwakilishwa na Mkurugenzi wa KfW nchini Tanzania, Vanessa Eidt.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Dk. Mwamba amesema mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji endelevu wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira, pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji katika maeneo ya Tunduma na Vwawa-Mlowo.

Amesema mradi huo utahusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji maji, kuunganisha wateja wapya, ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka, ununuzi wa magari ya majitaka (exhauster), pamoja na miundombinu ya usafi katika taasisi za umma kama shule.

Dk. Mwamba ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kusaidia miradi ya maendeleo nchini, akibainisha kuwa misaada hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika sekta za maji, afya, mazingira, usimamizi wa fedha za umma na usawa wa kijinsia.

Aidha, ameeleza kuwa miradi hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inayoelekea ukingoni mwezi Juni 2026, pamoja na Dira mpya ya 2050 na mipango ya maendeleo ya taifa inayolenga kuimarisha ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema mradi huo umefika wakati muafaka kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji linalosababishwa na ukuaji wa miji na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema utekelezaji wake utaimarisha usimamizi wa rasilimali za maji na kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi kwa wananchi, hatua itakayochochea maendeleo endelevu ya kiuchumi katika maeneo husika.

Naye Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Manuel Muller, pamoja na Mkurugenzi wa KfW nchini, Vanessa Eidt, wamesema Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, huku sekta ya maji ikiongoza kwa uwekezaji mkubwa.

Wamesema ushirikiano huo umeendelea kuimarisha huduma za kijamii na kuchangia maendeleo endelevu, wakiahidi kuendeleza mashirikiano hayo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments