Benki ya CRDB imetembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako watoto watano waliozaliwa kwa mpigo wanaendelea kupatiwa huduma za afya, na kuwafungulia akaunti watoto hao pamoja na wazazi wao, sambamba na kuwapatia zawadi mbalimbali za kusaidia maendeleo ya familia hiyo.
Katika ziara hiyo, Afisa Uendeshaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile, amemkabidhi bajaji mpya baba mzazi wa watoto hao, Simon Benjamin Mkwizu, pamoja na kumfungulia akaunti ya biashara, huku mama wa watoto hao, Bi. Victoria, akifunguliwa Akaunti ya Malkia.
Kupitia kitengo cha Huduma kwa Vijana (Youth Banking), benki hiyo imewafungulia watoto hao Akaunti ya Junior Jumbo na kuweka kiasi cha shilingi milioni 1.5 kwa kila mtoto kama mtaji wa awali wa maisha yao ya baadaye.
Kwa upande wa mama, amepatiwa shilingi milioni 2.5, ambapo shilingi milioni 1.5 zimewekwa kwenye akaunti na shilingi milioni 1 zimetolewa kwa ajili ya kusaidia kukuza mtaji wa biashara yake.




Aidha, baba wa familia hiyo ambaye ni afisa usafirishaji, amefunguliwa Akaunti ya Imbeju inayolenga wajasiriamali, na kuwezeshwa kwa bajaji mpya iliyokatiwa bima, ili kumsaidia kuongeza kipato na kuhudumia familia yake iliyoongezeka ghafla.
Benki hiyo pia imegharamia bima ya afya ya kiwango cha juu (premium health insurance) kwa mama na watoto wote, sambamba na mpango wa uwekezaji kupitia kitengo cha brokerage ambapo kila mtoto amenunuliwa hisa zenye thamani ya shilingi 500,000.
Kupitia programu ya iMBEJU iliyo chini ya CRDB Bank Foundation, baba wa familia atapatiwa mafunzo ya elimu ya fedha na ujasiriamali ili kumjengea uwezo wa kiuchumi katika malezi ya watoto hao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwile amesema benki hiyo imeamua kuisaidia familia hiyo kutokana na ongezeko la majukumu ya malezi, akisisitiza kuwa CRDB inaendelea kujikita katika huduma jumuishi za kifedha zinazowafikia wananchi wa rika na kipato mbalimbali.






Kwa upande wake, Mkwizu ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo mkubwa akisema utakuwa msaada muhimu katika kulea watoto hao, huku akiahidi kuwa balozi wa taasisi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, amesema msaada huo utarahisisha pia upokeaji wa michango kutoka kwa watu binafsi na taasisi, ambapo wale wanaolenga msaada wa muda mrefu watachangia kupitia akaunti za watoto, na wale wa matumizi ya haraka kupitia akaunti ya mama.
Amesema watoto hao, ambao sasa wanaendelea vizuri ikiwa ni siku ya sita tangu kuzaliwa, wameanza kuimarika na hawatumii tena mashine kutokana na huduma bora wanazoendelea kupatiwa hospitalini hapo.








