Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amemtaka Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kusimamia kwa karibu malipo ya wakulima wa kahawa ili kuwalinda dhidi ya ucheleweshaji wa fedha zao unaofanywa na baadhi ya kampuni zinazojihusisha na ununuzi wa zao hilo.
Kapinga, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, ametoa maelekezo hayo mapema wiki hii wakati akizungumza katika kikao na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Amesisitiza kuwa zao la kahawa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na chanzo kikuu cha maisha ya wananchi wengi, hivyo Serikali haitavumilia kuona wachache wanaitia doa sekta hiyo kwa uzembe au kwa kushindwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa sheria na kanuni zinazolenga kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati.




Katika maelekezo yake, Waziri Kapinga amemwagiza Afisa Ushirika wa wilaya hiyo kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao bila visingizio, huku akiwataka watumishi wa umma kutotumia masuala ya ukomo wa malipo kama kisingizio cha kuwakandamiza wakulima.
Aidha, Waziri Kapinga amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kufanya tathmini upya ya kampuni ya Mamba Coffee ili kubaini kama inastahili kuendelea kupewa kibali cha kununua kahawa katika wilaya hiyo, kufuatia malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima. Amesema kuchelewesha malipo ni sawa na kuwarudisha nyuma wakulima pamoja na kudhoofisha maendeleo yao.


Vilevile, amewahimiza viongozi wa vyama vya ushirika kukaa vikao mapema na kufanya maamuzi muhimu kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo, hatua itakayosaidia kuzuia migogoro inayoweza kuepukika.
Pia ametoa onyo kali dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za ushirika, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kutumia fedha hizo kwa maslahi binafsi, akisema vitendo hivyo havitavumiliwa kabisa.








