Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), chini ya Mwenyekiti wake, Mhandisi Romanus Mwang’ingo, imefanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kujionea hali ya upatikanaji wa huduma ya maji na kufuatilia maboresho yanayoendelea kutekelezwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Mwang’ingo alisema lengo kuu ni kuhakikisha DAWASA inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwapatia wananchi huduma bora, salama na endelevu ya maji.
“Tumetembelea maeneo mbalimbali na tumeshuhudia kuwa huduma ya maji imeendelea kuimarika, hususan katika maeneo yaliyokuwa na changamoto hapo awali kama Msakuzi, Mshikamano na Msumi. Kwa sasa wananchi wengi wanapata huduma kwa kiwango cha kuridhisha,” amesema Mhandisi Mwang’ingo.


Ameongeza kuwa, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna maeneo yenye changamoto za huduma ya maji, huku akibainisha kuwa DAWASA imeendelea kuyatambua na kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapatiwa huduma kwa uhakika.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amewahimiza wananchi kushirikiana na Mamlaka kwa kutunza miundombinu ya maji na kulipia huduma kwa wakati ili kuwezesha kuendelea kuboresha na kupanua huduma hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Msakuzi, Miriam Kiuko, amesema hali ya upatikanaji wa maji imebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo ambalo limeongeza furaha na kurahisisha shughuli za kila siku za wananchi.
“Kwa sasa tunapata maji kwa wingi na shughuli za maendeleo zinaendelea vizuri. Tunawashukuru DAWASA kwa kutusikiliza na kushughulikia changamoto zetu kwa haraka kila tunapowasilisha malalamiko,” amesema Kiuko.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Bodi ya Wakurugenzi wa DAWASA za kufuatilia utekelezaji wa miradi na kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kuboreshwa kwa manufaa ya wananchi wa Dar es Salaam na maeneo jirani.






