Thursday, February 12, 2026
spot_img
HomeAfyaDk. Samia kuwa kinara wa Afya ya Mama na Mtoto Afrika

Dk. Samia kuwa kinara wa Afya ya Mama na Mtoto Afrika

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amependekezwa kuteuliwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika (AU) katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo.

Kupendekezwa kwa Dk. Samia kushika wadhifa huo, kunaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.

Hata hivyo, hii haitakua mara ya kwanza kwa Dk. Samia, kupewa nafasi ya kuwa kinara wa sekta mbalimbali, hadi sasa ni kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika na duniani, nafasi aliyoishika baada ya mafanikio ya ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.

Uteuzi wa mkuu huyo wa nchi katika wadhifa huo, unatarajiwa kufanyika kati ya Februari 14 na 15, 2026, katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za AU, Addis Ababa nchini Ethiopia, ambao tayari Dk Samia ameshasafiri kwenda kushiriki.

Ukiacha uteuzi huo, katika safari hiyo, Februari 13, Dk. Samia atashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), utakaofanyika chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, kisha atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Abiy Ahmed.

Mkuu huyo wa nchi, atafanya mazungumzo ya pande mbili na Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Russell Dlamini, Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Sidi Tah, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments