Wakulima nchini wanatarajiwa kunufaika na soko la uhakika, upatikanaji wa mikopo, pembejeo na bei yenye tija kupitia mfumo wa kilimo cha mkataba unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), huku wakihimizwa kuachana na mikataba ya mdomo inayosababisha migogoro na hasara.
Mratibu wa Kilimo cha Mkataba wa COPRA, Rehema Msauge, alisema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo ya kanuni za kilimo cha mkataba yaliyowakutanisha wadau wa sekta hiyo, wakiwemo wakulima na taasisi za kifedha zinazojihusisha na mfumo huo.
Alisema kilimo cha mkataba kwa mazao yote yasiyo na bodi maalumu kinalenga kulinda maslahi ya wakulima na wanunuzi kwa kuhakikisha makubaliano yote yanatambulika kisheria na kusimamiwa ipasavyo.




Msauge alisema mfumo huo unamwezesha mkulima kumfahamu mnunuzi wa mazao yake kabla ya mavuno, jambo linalompa uhakika wa soko na kumwezesha kupanga uzalishaji wake kwa tija zaidi.
Aliongeza kuwa kuwepo kwa mikataba inayotambulika kisheria kunawapa wakulima fursa ya kupata mikopo kutoka taasisi za fedha, pembejeo na mitaji kutoka kwa wadau wa maendeleo, huku pia kukichochea uzalishaji wa mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
Aidha, alisema COPRA huweka bei ya kuanzia ya mazao baada ya kufanya tathmini ya gharama halisi za uzalishaji na mwenendo wa soko, kwa lengo la kuhakikisha mkulima anapata kati ya asilimia 75 na 80 ya bei ya mwisho ya mazao husika.




“Hivyo wakulima na wafanyabiashara wanapaswa kuepuka makubaliano ya mdomo. Ni lazima wawe na mikataba ya maandishi inayotambulika kisheria, ambayo mamlaka itaisimamia ili kuondoa mazingira ya wakulima kudhurumiwa na kupata hasara,” alisema.
Alifafanua kuwa kabla ya kusainiwa kwa mkataba, wahusika wanapaswa kufikia makubaliano ya awali yanayobainisha eneo la uzalishaji, kusajili taarifa kwenye mfumo wa COPRA, kuandaa rasimu ya mkataba, kuuhakiki na hatimaye kuusajili rasmi pamoja na kutambuliwa na serikali za mitaa.
Kuhusu gharama za usajili, alisema mkulima mdogo atalipa Sh10,000, mkulima wa kati Sh20,000 na mkulima mkubwa Sh40,000.Alisema vyama vya ushirika (AMCOS) vyenye wanachama kati ya 20 na 50 vitalipa Sh100,000, vyenye wanachama 51 hadi 200 vitalipa Sh250,000, huku vyenye wanachama 201 na kuendelea vikitozwa Sh500,000.
Msauge alionya kuwa ukiukwaji wa masharti ya mikataba ya kilimo cha mkataba utachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, mtu binafsi anayekiuka masharti ya mkataba anaweza kutozwa faini ya kati ya Sh1 milioni na Sh5 milioni au kifungo cha mwaka mmoja hadi miwili jela, au adhabu zote mbili kwa pamoja. Taasisi zitakazokiuka masharti hayo zitatozwa faini ya kati ya Sh5 milioni na Sh10 milioni.
Alisisitiza kuwa matumizi ya mikataba rasmi yataongeza uwazi katika biashara ya mazao, kuimarisha uaminifu kati ya wakulima na wanunuzi na kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia biashara yenye tija na inayozingatia sheria.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Joel Lunyungu kutoka Shirika la CARE International, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka kwa kuwa yatawasaidia wakulima kuondokana na mikataba yenye utata.





