Friday, February 13, 2026
spot_img
HomeHabariOSHA italipunguzia Taifa mzigo wa fidia na matibabu-Kamati ya Bunge

OSHA italipunguzia Taifa mzigo wa fidia na matibabu-Kamati ya Bunge

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imesema majukumu ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yakitekelezwa ipasavyo yatalipunguzia Taifa mzigo wa kuhudumia wananchi wanaoweza kuumia au kupata magonjwa yatokayo na kazi.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Chakoma, alipokuwa akihitimisha mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa wajumbe wa Kamati hiyo Februari 12, 2026.

Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yamefanyika bungeni Jijini Dodoma ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati hiyo katika kikao cha Januari 19, 2026 OSHA ilipowasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu yake. Mafunzo hayo yanalenga kuiwezesha Kamati hiyo kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kuisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) na Taasisi chini yake ikiwemo OSHA.

Chakoma ameipongeza Taasisi ya OSHA kwa jitihada inazofanya kutekeleza majukumu yake ikiwemo kutoa mafunzo kwa waaajiri na wafanyakazi, kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya ukiwemo uchunguzi wa afya za wafanyakazi katika hatua mbalimbali. 

“Niendelee kuwapongeza pamoja na kuwashukuru kwa mafunzo haya ambayo yamewafungua wabunge wengi na kimsingi ni mafunzo mazuri ambayo ukiyaangalia kwa haraka haraka unaweza kudhani ni kwa ajili ya maeneo ya kazi tu lakini kiukweli unaweza kuyatumia hata katika mazingira ya nyumbani kwenye hatari tofauti tofauti,” ameeleza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuongeza:

“Mafunzo haya ni kwa ajili ya kuimarisha afya za wafanyakazi na wananchi kwa ujumla na sote tunakuballiana kwamba OSHA ipo kwa ajili ya kuliokoa Taifa ambapo ikifanya kazi yake sawa sawa kwa mujibu wa utaratibu waliotueleza hapa ama hakika tutakuwa tunaliokolea Taifa letu mzingo mzito wa kuwatibia wagonjwa ama kuwapa fidia wafanyakazi waliomia kazini.”

Sambamba na kuipongeza OSHA kwa kutoa mafunzo mazuri, Kamati hiyo imeitaka OSHA kuwashauri wamiliki wa sehemu za kazi kutumia teknolojia na mitambo ya kisasa iliyosanifiwa katika namna inayopunguza athari nyingi za kiusalama na kiafya wakitolea mfano wa vipando (lift) zilizopo katika majengo marefu katika miji mbalimbali hapa nchini.

Aidha, Kamati hiyo imependekeza elimu ya masauala ya usalama na afya kutolewa kwa wabunge wote pamoja na wanachi mbalimbali wakiwemo wakulima wadogo wadogo hususan wanaojishughulisha na kilimo cha tumbaku mkoani Tabora.

“Tangu nilipoingia kwenye hii Kamati na kujua kazi zinazofanywa na OSHA natamani kuwaona kila mahali na kupitia mafunzo yetu ya leo OSHA wametoa elimu kubwa sana japo hatukuwa na muda wa kutosha,” amesema Katani Ahmad Katani, Mjumbe wa Kamati.

“Niwapongeze OSHA kwa mafunzo mazuri na niungane na wenzangu kusema kuwa mafunzo haya ni muhimu sana na yanaweza kutusaidia sana katika maisha yetu ya kila siku na niombe tuendelee kupatiwa mafunzo kama haya,” ameeleza Mariam Kisangi ambaye ni Mjumbe wa Kamati.

OSHA ni miongoni mwa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Miongoni mwa majukumu ya msingi ya OSHA ni kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa waajiri, wafanyakazi na umma kwa ujumla.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments