Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dk James Mwainyekule, leo, 4 Machi, 2026 ameshiriki kikao cha ngazi ya juu cha wamiliki wa kampuni za bidhaa za mafuta aina ya petroli nchini (OMCs) kilichoitishwa na Waziri wa Nishati Deogratias Ndejembi ili kujadili mikakati ya iliyowekwa na serikali kuimarisha hali ya upatikanaji wa mafuta hususani kipindi hiki cha migogoro inayoendelea baina ya nchi za Irani na Marekani.
Wakati wa kikao hicho, Waziri Ndejembi aliwahakishia ushirikiano thabiti wamiliki wa kampuni za mafuta nchini (OMCs) na kuwaeleza kuwa Serikali imechukua hatua stahiki kuhakikisha changamoto zinazotokana na mzozo huo zinatatuliwa.


“Serikali iko macho, imejipanga na imefanya kila linalowezekana kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa mafuta, na tutawapatia ishikiano wa hali ya juu, ni rai yangu kwa kila mmoja kufuata sheria za nchi.”
Aidha, aliwaomba kutoa ushirikiano wakati wote kwa kuhakikisha kuwa watanzania wanapata huduma za mafuta bila kikwazo chochote.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, nae alitumia fursa hiyo kuwahakikishia watoa huduma hao kuwa wataendelea kupokea ushirikiano wa kutosha katika shughuli zao na kusisitiza kuwa yeyote atakayekiuka utaratibu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.






