Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeingia makubaliano na Taasisi ya Ali Kimara Disease Foundation (AKRDF) ya kupokea Sh. milioni 100 kwa ajili ya kuendesha tafiti kuhusu magonjwa adimu nchini.
Katika hatua hiyo, Serikali imeahidi kuwezesha upatikanaji wa rasilimali ili kuimarisha ukusanyaji wa takwimu sahihi, kuboresha utambuzi wa magonjwa hayo pamoja na kuandaa sera na miongozo inayozingatia ushahidi wa kisayansi.
Akizungumza Machi 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Magonjwa Adimu 2026 lililoandaliwa kwa ushirikiano wa MUHAS na AKRDF, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za chuo hicho katika kuwa kitovu cha ubora, ubunifu na utafiti kwa maendeleo ya taifa na ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema MUHAS ina wajibu wa kuongoza tafiti na kuzalisha wataalamu mahiri katika sekta ya afya. Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za rufaa na kuimarisha mifumo ya matunzo inayounganisha huduma za msingi na zile za kibingwa.


Kwa mujibu wa Dk. Magembe, duniani kuna zaidi ya magonjwa adimu 7,000 yanayoathiri takribani watu milioni 400, huku asilimia 80 ya magonjwa hayo yakisababishwa na vinasaba. Wastani wa mtu mmoja kati ya 2,000 huathirika.
Ameongeza kuwa nchini Tanzania, inakadiriwa kuwa asilimia sita ya wananchi wanaweza kuwa na aina fulani ya ugonjwa adimu.
Dk. Magembe ametaja baadhi ya magonjwa adimu yanayoonekana zaidi kuwa ni selimundu, hemofilia, tawahudi, lupus erythematosus na Gaucher. Kwa ujumla, magonjwa hayo yanaathiri kati ya watu milioni tatu hadi nne nchini, wengi wao wakiwa watoto, hali inayoonesha kuwa suala hilo ni kipaumbele cha kitaifa kinachohitaji mikakati madhubuti.
Akitoa mfano wa selimundu, amesema huduma zake zinapatikana katika mikoa yote na zaidi ya asilimia 80 ya hospitali za wilaya, hatua inayolenga kuhakikisha wagonjwa wanagunduliwa mapema na kupatiwa huduma jumuishi kulingana na mahitaji yao.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya, amesema chuo kinatambua jukumu lake katika utoaji wa elimu, utafiti na huduma zinazohusu magonjwa adimu.


Ametaja changamoto zilizopo kuwa ni pamoja na uhaba wa vipimo vya vinasaba, gharama kubwa za uchunguzi pamoja na utegemezi wa maabara za nje ya nchi.
Ameongeza kuwa kupitia tafiti, ubunifu na ushirikiano na wadau mbalimbali, chuo kinaendelea kutafuta suluhisho endelevu yatakayotekelezwa ndani ya mfumo wa afya nchini.
“Kongamano hili limeandaliwa kama jukwaa la kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuibua mapendekezo yatakayobooresha utambuzi, matibabu na ubora wa maisha ya wagonjwa. Pia litatumika kusikiliza maoni ya wagonjwa na familia zao na kujadili namna bora ya kuimarisha rufaa kuanzia ngazi ya msingi hadi huduma za juu,” amesema Prof. Balandya.

Naye Mwenyekiti wa AKRDF, Sharifa Mbarak, amesema matokeo ya tafiti hizo yanatarajiwa kuleta maboresho chanya kwa watoto na jamii kwa ujumla, hasa yatakapoingizwa katika sera za afya.
Ameeleza kuwa makubaliano na MUHAS yanalenga kuanzisha tafiti mahususi, akibainisha kuwa kwa sasa watoto wenye magonjwa adimu hawatambuliwi ipasavyo katika mifumo ya bima ya afya, hivyo wanahitaji msaada zaidi.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Magonjwa Adimu: Ni Zaidi ya Tunavyoweza Kufikiria,” inalenga kuhamasisha jamii kulitambua suala hilo kama ajenda ya kijamii, kielimu, kiutafiti na kisera inayohitaji ushirikiano wa wadau wote.








