Friday, March 13, 2026
spot_img
HomeElimuRais Samia aleta mapinduzi ya elimu kwa kujenga Sekondari ya Iziwa

Rais Samia aleta mapinduzi ya elimu kwa kujenga Sekondari ya Iziwa

Wananchi wa Kata ya Iziwa wameeleza kufarijika na ujenzi wa Shule ya Sekondari Iziwa uliotekelezwa kupitia dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.‎‎‎

Ujenzi wa shule hiyo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 950 na umeanza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu eneo hilo.‎‎Mwanafunzi wa shule hiyo, Gerson Alex, amesema ujenzi wa shule hiyo umeondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule hali ambayo awali ilisababisha baadhi yao kuacha masomo.‎‎

“Nipende kumshukuru Rais Samia na serikali kwa ujumla kwa sababu wamefanya mambo makubwa katika Iziwa hii, tulikuwa tunatembea kwa umbali mrefu na changamoto nyingi na hiyo ikapelekea wanafunzi wengi kuacha shule lakini pia kupoteza ndoto zao,” amesema Gerson Alex.

‎‎Mkuu wa shule hiyo, Rehema Masige, amesema shule hiyo ilianza kujengwa mwaka 2022 na kukamilika Januari 9, 2023 ambapo wanafunzi wa kidato cha kwanza walianza masomo rasmi.‎‎‎

“Shule hii ilianza kujengwa mwaka 2022 kama shule mpya na ilikamilika 2023, tarehe 9 Januari 2023 kidato cha kwanza kilianza ambapo tulikuwa na madarasa nane, ofisi nne ambazo zipo kwenye madarasa, lakini pia jengo la utawala lenye ofisi nane. Tulikuwa na jengo lenye maabara tatu, maabara ya fizikia, baiolojia na kemia, lakini pia tuna jengo la ICT ambalo ni computer room, pia tuna jengo la maktaba,” amesema Masige.

‎‎‎Ameongeza kuwa shule hiyo ilijengwa kwa awamu tofauti za ufadhili wa serikali.‎“Shule mpya imejengwa kwa milioni 470, baadaye 2023 mwishoni tukaongezewa milioni 100 ambazo tumejenga nyumba ya mwalimu na sasa walimu wanaishi.‎‎‎

Lakini baada ya kukamilika nyumba ya mwalimu tukaongezewa tena milioni 380 kwa ajili ya utanuzi wa shule kidato cha tano na sita. Fedha hizo zimetumika kujenga mabweni mawili, bweni la wasichana, madarasa manne na matundu kumi ya vyoo na miundombinu hii yote inatumika,” amesema.‎‎‎

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamesema ujenzi wa shule hiyo umeondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.‎‎‎“Rais wetu namshukuru sana kwa kazi aliyofanya kama shule. Watoto wetu walikuwa wanaenda mbali sana, mimi kama mzazi namshukuru sana Rais na Diwani wetu kwa shule hii,” amesema mkazi wa Iziwa, Sensa Jason.‎‎‎

Naye Matilda Petro amesema shule hiyo imekuwa faraja kwa wazazi na wanafunzi wa eneo hilo.‎‎“Kwakweli tunamshukuru Rais wetu mama Samia kwa kutuletea shule nzuri katika kijiji chetu, awali watoto wetu walikuwa wanaenda shule mbali, sasa hivi tumepata shule nzuri tena iko karibu. Tunamshukuru sana,” amesema.‎‎‎

Kwa upande wake, mwanafunzi Stephanie Simon amesema uwepo wa maabara za sayansi shuleni hapo unawasaidia wanafunzi kufikia ndoto zao za taaluma.‎‎‎“Ndoto yangu ni kuwa injinia, kwa uwekezaji mkubwa katika hizo maabara za sayansi inanisaidia kutimiza ndoto zangu kwa urahisi.

Namshukuru Rais Samia kwa sababu kila kitu kipo, sipati changamoto yoyote,” amesema.‎Diwani wa Kata ya Iziwa, Kephas Mwasote, amesema ujenzi wa shule hiyo ni jambo ambalo wananchi hawatalisahau.‎‎‎“

Kwa kitendo alichotufanyia Iziwa hatutasahau maishani mwetu. Kwa historia tumeanza kujenga shule katika kata zingine lakini kwetu hakuna shule. Tulifika mahala ikaonekana hakuna mtu wa kutusaidia, ni neema ya Mheshimiwa Rais iliyokuja kutuokoa. Kama ulivyoona majengo haya yote ni neema ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments