Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amewataka watumishi wa Wizara ya Nishati kuendelea kuhamasisha na kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ili kufanikisha ajenda ya kitaifa inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema ajenda hiyo tayari imeanza kuzaa matunda, hali iliyochangia Tanzania kupata kutambuliwa kimataifa, ikiwemo ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mhandisi Luoga alitoa kauli hiyo Machi 18, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati, kwa niaba ya Makatibu Wakuu wa wizara hiyo.




Ameeleza kuwa katika mkutano wa SADC uliofanyika hivi karibuni, Tanzania ilipongezwa kwa hatua kubwa iliyofikia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Alinukuu pia hotuba ya Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, ambaye aliitambua na kuipongeza Tanzania kwa juhudi hizo, huku nchi wanachama zikihimizwa kuunga mkono hatua hizo kupitia maazimio ya pamoja.
Kutokana na mafanikio hayo, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti katika kusukuma mbele ajenda hiyo, pamoja na kuwapongeza watumishi wa Wizara ya Nishati kwa juhudi zao katika kuboresha afya za wananchi na kupunguza uharibifu wa mazingira.




Katika kikao hicho, ambacho kilijadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mhandisi Luoga amewasisitiza wajumbe kuhakikisha vipaumbele vyote muhimu vinapatiwa fedha za kutosha ili kuwezesha utoaji bora wa huduma kwa wananchi.
Aidha, amewataka watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuepuka vitendo vya utoro na rushwa, na kuendeleza uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa TUGHE ngazi ya mkoa na tawi la Nishati, pamoja na wawakilishi kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, ukiwa na lengo la kuimarisha utendaji kazi na ustawi wa sekta hiyo muhimu.








