Shirikisho la Soka la Ghana (GFA) limetangaza rasmi kuachana na kocha wa timu ya taifa ya wanaume, Otto Addo, mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Ujerumani.
Kupitia taarifa rasmi, GFA imemshukuru Addo kwa mchango wake ndani ya timu hiyo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake yajayo, huku ikieleza kuwa mwelekeo mpya wa benchi la ufundi utatangazwa hivi karibuni.
Addo anaondoka baada ya kuitumikia Ghana kwa kipindi cha miaka miwili na siku 16, ambapo aliiongoza timu katika michezo 22. Katika kipindi hicho, alifanikiwa kushinda mechi 8, kutoka sare 5 na kupoteza michezo 9, takwimu zinazoonyesha asilimia 36.3 ya ushindi.
Uamuzi huo unakuja katika wakati nyeti kwa timu ya taifa ya Ghana, Black Stars, ambayo imebakiza siku 72 pekee kuelekea Kombe la Dunia 2026.
Hatua hiyo inaifanya GFA kuanza harakati za haraka za kusaka kocha mpya atakayechukua jukumu la kuiandaa timu hiyo kwa mashindano hayo makubwa ya kimataifa.




