Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kushughulikia malalamiko yote ya wananchi yanayowasilishwa kupitia programu ya Sema na Waziri katika Kituo cha Huduma kwa Mteja, kwa weledi, ufanisi na uwajibikaji.
Akizungumza Aprili 22, 2026, Mtumba jijini Dodoma wakati wa programu hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Juma Homera amesisitiza kuwa Wizara hiyo ina wataalamu wa kutosha, wenye ujuzi na ari ya kufanya kazi, ambao wako tayari kushughulikia changamoto za Watanzania popote walipo nchini.
Dk.Homera ameeleza kuwa programu hiyo ni endelevu, ambapo wananchi wataendelea kupata fursa ya kuwasilisha malalamiko yao mara mbili kwa mwezi na wizara hiyo itahakikisha inatoa mrejesho wa kina kuhusu migogoro na changamoto zote zinazowasilishwa, ili kuongeza imani ya wananchi kwa huduma za serikali.


“Hatuchagui kero, tunapokea kero zote, tunasikiliza changamoto zote, na tunaendelea kuzifanyia kazi kwa bidii,” amesema Dk. Homera.
Ameongeza kuwa Wizara hiyo, imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususani waliopo maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto za kisheria zinazowakabili ikiwamo kupokea maoni na ushauri, kwa lengo la kuboresha huduma na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.
Aliwataka wananchi wenye shida inayohitaji kuzungumza na Waziri au kupata msaada wa kisheria, kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Wizara hiyo, kupiga simu bure kwa namba 0262 160 360 au 0800 004 004 ama kutuma ujumbe kwa njia ya WhatsApp kwa namba 0739 101 910, huduma zinazotolewa jumatatu hadi ijumaa jioni.





