Rais wa Marekani Donald Trump aliondolewa haraka jukwaani na walinzi wa Idara ya Ulinzi wa Rais kufuatia taarifa za kusikika kwa milio ya risasi wakati wa hafla ya chakula cha jioni cha waandishi wa habari wa Ikulu ya White House iliyofanyika Washington, DC, jana Jumamosi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais JD Vance pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Mawaziri waliokuwepo walikimbizwa nje kwa usalama.

Taarifa kutoka vyanzo vya karibu zilieleza kuwa Trump yuko salama, na kwa mujibu wa afisa wa serikali, viongozi wengine wote pia hawakupata madhara.
Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wake wa kijamii, Trump aliwapongeza maafisa wa usalama kwa kuchukua hatua za haraka na kuonyesha ujasiri mkubwa.
Aidha, alieleza kuwa alipendekeza “TUENDELEE NA SHUGHULI,” lakini akasisitiza kuwa ataendelea kufuata maelekezo ya vyombo vya usalama.










