HomeHabari‎Bodi ya DAWASA yasisitiza kukamilika kwa wakati ufungaji pampu mpya za maji

‎Bodi ya DAWASA yasisitiza kukamilika kwa wakati ufungaji pampu mpya za maji

‎Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhandisi Romanus Mwang’ingo, imekagua zoezi la ufungaji wa pampu mpya za kusukuma maji ghafi katika Mtambo wa Kuzalisha Maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi, mkoani Pwani na kusisitiza ukamilishaji wake kwa wakati.

‎Pampu hizo, zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 16, zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa uzalishaji na usambazaji wa maji, na kuboresha huduma kwa zaidi ya wakazi milioni saba wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

‎Katika ziara hiyo, Bodi pia ilipokea taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa kudhibiti upotevu wa maji katika maeneo ya Mlandizi na Kibaha, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa DAWASA wa kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


‎Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Mwang’ingo aliwataka watumishi wanaosimamia mradi huo kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kujituma na kuhakikisha ufungaji wa pampu unakamilika kwa wakati.

‎ “Niendelee kuwatia moyo watumishi mnaoendelea na kazi hii kuifanya kwa weledi na kuikamilisha kwa wakati ili wananchi wapate huduma bora na endelevu ya majisafi na salama. Hili ni jukumu letu sote,” amesema Mhandisi Mwang’ingo.

‎Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kwa wakati kutakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa maji na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.

‎DAWASA inaendelea kutekeleza maboresho mbalimbali ya miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama kwa uhakika na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji yanayoongezeka.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments