Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imesema Mahakama Kuu iliwapa
uhalali kisheria wa kuwapo na kufanya kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mjumbe wa Tume, Prof. Ibrahim Juma, amesema uhalali wa Tume hii ulithibitishwa na Mhakama Kuu ya Tanzania.
“Wengi wamekuwa wakihoji uhalali wa tume yetu. Nataka kuweka rekodi sawa. Mahakama Kuu ya Tanzania, katika Shauri Namba 12 la Mwaka 2025, ilitoa uamuzi wa wazi kuwa Rais ana mamlaka kikatiba kuunda tume za uchunguzi, na kwamba Tume hii imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32,” amesema Prof. Juma.
Ameongeza kuwa uamuzi huo ulitolewa baada ya baadhi ya watu kufungua kesi mahakamani kupinga uwepo wa Tume. “Jaji amesema wazi: Tume hii ni halali. Kazi zake ni halali. Ushahidi uliokusanywa ni halali.”
Prof. Juma ameeleza kuwa kinga hiyo ya kisheria ndiyo iliyoiwezesha Tume kuwaita na kuwahoji wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa, makamanda wa polisi, viongozi wa vyama vya siasa, na wananchi wapatao 63,603 bila woga.
“Tusingeweza kukamilisha kazi hii kama tusingekuwa na ngao ya kisheria kutoka Mhimili wa Mahakama,” amesisitiza.
Tume imeshakabidhi Ripoti yake kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 23 Aprili, 2026.
“Uhalali wa ripoti hii haukutoka Ikulu pekee ulithibitishwa na Mahakama. Kilichobaki sasa ni Watanzania kuisoma, kuijadili, na taasisi husika kuchukua hatua stahiki,” amethibitisha Prof. Juma.




