Uchumi wa Tanzania unatarajiwa kunufaika na fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati kufuatia kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Maelewano (MoU) kati ya Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) na National Export Promotion Council of Belarus.
Makubaliano hayo yaliyoshuhudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb), yanatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta za kilimo, viwanda na usindikaji, madini, nishati, teknolojia, usafirishaji, vifaa tiba pamoja na upanuzi wa masoko ya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kombo alisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na kuimarisha nafasi ya sekta binafsi katika biashara na uwekezaji.




“Makubaliano haya yanaweka msingi imara wa kufungua fursa mpya za ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili,” alisema Balozi Kombo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov, alisema ushirikiano huo unalenga kuzaa matokeo ya vitendo yatakayoongeza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.
“Tuko tayari kuendeleza ushirikiano wa vitendo utakaoleta matokeo chanya kwa mataifa yetu,” alisema Ryzhenkov.




Rais wa TNCC, Bw. Vicent Minja, alisema MoU hiyo ni daraja muhimu la kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji, huku akisisitiza umuhimu wa utekelezaji ili makubaliano hayo yatoe manufaa ya moja kwa moja kwa uchumi.
“Sasa tunahitaji kuhamisha makubaliano haya kutoka kwenye nyaraka kwenda kwenye utekelezaji wenye matokeo,” alisema Minja.
Kupitia ushirikiano huo, Tanzania na Belarus zinatarajiwa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kuongeza ubadilishanaji wa teknolojia na maarifa, kuchochea miradi ya pamoja na kuendeleza diplomasia ya uchumi kupitia masoko mapya na fursa za kimataifa.







