Mwili wa raia wa Marekani, Ashly Robinson (31), unatarajiwa kuzikwa Jumanne Mei 5, 2026 katika jimbo la New Jersey kufuatia kifo chake kilichotokea visiwani Zanzibar.
Taarifa zinaeleza kuwa Ashly, aliyekuwa nchini Tanzania kwa matembezi ya kitalii, alikutwa amefariki dunia Aprili 10, 2026 ndani ya chumba cha hoteli baada ya kudaiwa kujinyonga.
Mwanzoni mwa wiki hii, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa mwili wa marehemu ulirejeshwa kutoka Tanzania na kukabidhiwa kwa familia yake Ijumaa iliyopita kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Inaelezwa kuwa Ashly alikuwa ameambatana na mpenzi wake, Joe McCann, ambaye alimchumbia siku sita kabla ya tukio hilo wakati wakiwa visiwani humo.
Kifo hicho kimeibua masikitiko kwa familia na marafiki, huku taarifa zaidi kuhusu chanzo kamili cha tukio hilo zikiendelea kufuatiliwa.





