*Yajipanga Kubeba Suluhu ya Uhaba wa Gesi hiyo Duniani*
*Helium One Global Yasema Akiba ya Songwe ina Thamani Kubwa Kijiolojia*
*Mradi Kuanza Kutekelezwa baada ya Miezi 18, Zaidi ya Dola Milioni 60 tayari Zimewekezwa*
*Serikali Kumiliki Asilimia 17 ya Hisa kupitia Kampuni ya Ubia ya Songwe Helium Limited*
📍*Songwe*
Tanzania imeanza rasmi Safari Mpya ya Kihistoria ikiingia kwenye ramani ya dunia kama Mzalishaji na Msambazaji wa kimkakati wa Gesi ya Helium. Hatua hiyo inafuatia baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Uchimbaji wa gesi hiyo baina ya Serikali na kampuni ya Helium One Global Limited kupitia Kampuni ya Ubia ya Songwe Helium Limited, katika hafla iliyofanyika Mei 2, 2026 Mkoani Songwe.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akizungumza katika hafla hiyo na kueleza kuwa, uzalishaji wa helium duniani kwa sasa unatawaliwa na nchi chache, hususan Marekani na Qatar, zinazochangia zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wote, huku Urusi, Algeria, Canada, China na Poland zikichangia kwa kiwango kidogo. Ameongeza kuwa mahitaji ya gesi hiyo tayari yamevuka futi za ujazo bilioni 6 kwa mwaka na yanatarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya bilioni 8.5 ifikapo mwaka 2030 ambapo kwa Tanzania kampuni za Helium One Global Limited na Noble Helium zimepiga hatua kubwa katika shughuli za utafiti wa gesi hiyo.
Ameeleza kuwa, mradi wa Southern Rukwa ni wa kimkakati unaoiwezesha Tanzania kuingia kwenye soko lenye thamani kubwa na ushindani mdogo na kuiweka katika nafasi ya kuathiri mwelekeo wa soko la helium duniani, huku ikitarajiwa kuwa sehemu ya suluhisho la uhaba wa gesi hiyo duniani na kueleza kwamba, uchimbaji wa helium utakwenda sambamba na gesi ambata kama hydrogen ambapo manufaa yake kimapato yatatenganishwa.




Aidha, Dkt. Kiruswa amefafanua kwamba kupitia mkataba huo, Serikali itamiliki asilimia 17 ya hisa katika kampuni ya ubia ya Songwe Helium Limited, hatua inayoiwezesha kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kimkakati na kunufaika na mapato ya mradi kwa manufaa ya Taifa na wananchi.
‘’Huu ni utekelezaji halisi wa falsafa ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa rasilimali za nchi lazima ziwe chanzo cha ustawi wa taifa,’’ amesema Dkt. Kiruswa.
Akizungumzia manufaa mengine ya mradi huo amesema utachangia ajira kwa vijana wa eneo husika na taifa kwa ujumla, fursa za kibiashara kwa wazawa kupitia huduma za ugavi, uboreshaji wa miundombinu, mapato kwa Serikali na fedha za kigeni na uboreshaji wa miundombinu muhimu kama barabara na huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Helium One Global Limited, Lorna Blaisse amesema utiaji saini huo ni hatua muhimu kwa Tanzania na soko la helium duniani, akibainisha kuwa mradi una akiba yenye thamani kubwa na unaelekea kwenye uzalishaji wa kibiashara baada ya mafanikio ya uchimbaji kisima mwaka 2024 ambacho kilipelekea ugunduzi wa helium katika kisima cha Itambula West-1.




‘’Katika upimaji wa kisima uliopanuliwa robo ya tatu ya 2024, kisima cha ITW-1 kilirekodi helium yenye mkusanyiko wa asilimia 5.5 hadi juu ya ardhi, na hadi asilimia 7.6 kutoka miamba ya Karoo iliyovunjika na miamba ya Basement iliyopasuka,’’ amesema
Amesema baada ya utiaji saini wa leseni ya uchimbaji, kampuni ya Songwe Helium Ltd itaendelea na hatua za uendeshaji kuelekea uzalishaji wa kwanza wa kibiashara wa heliamu. Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kukamilisha mipango ya maendeleo; mfumo wa usimamizi wa tathmini ya athari za mazingira na jamii; kubuni miundombinu, na kununua vifaa vya uchakataji na usafirishaji wa bidhaa.
Pia, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake na kuridhia muundo wa ubia unaohakikisha nchi inanufaika na rasilimali zake, akibainisha dhamira ya kuzalisha helium ya Tanzania kwa uwajibikaji na ubora wa juu kwa soko la dunia.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Wizara ya Madini Prof. Sifuni Mchome amesema kupitia utaratibu wa Serikali kumiliki hisa huru zisizohafifishwa thamani, Serikali inashiriki moja kwa moja katika miradi ya madini, inapata faida kupitia gawio, mrabaha,kodi na tozo mbalimbali, inashiriki maamuzi ya kimkakati, kulinda mapato na maslahi ya wananchi kwa uwazi na uwajibikaji.
” Tulijadiliana kwa utaratibu mzuri bila kugombana na tumefika kwenye hatua ya kila mmoja apate, na leo tuko hapa kuweka wazi na kila mmoja ashuhudie,” amesema Prof. Mchome.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Jabiri Makame amesema Mkoa huo ni wa kimkakati ukiwa na utajiri wa Madini mbalimbali yakiwemo ya rare earth elements ambao utafiti wake unaendelea.
” Tunaipongeza Wizara ya Madini kwa kutafsiri kwa vitendo. Kwetu sisi suala la kuwasaidia wawekezaji kutekeleza mradi Kwa mafanikio ni kipaumbele cha kwanza,” amesema Mhe. Makame.
Helium ni gesi ya kipekee sana duniani kwa sababu haina mbadala wake na matumizi yake ni ya kimkakati kwa maisha ya kisasa ya binadamu; inatumika katika vifaa vya tiba kama MRI, uzalishaji wa vifaa vya kielektroniki na teknolojia za kidigitali; sekta ya anga; ulinzi na tafiti za kisayansi, teknolojia za kisasa kama fibre optics na quantum computing.
Mradi huo unatekelezwa katika eneo la kilomita za mraba 480 ukiwa zaidi katika Mkoa wa Songwe Wilaya ya Momba na sehemu ndogo ikiingia Mkoa wa Rukwa.




