Na Imani Nathaniel
Wadau kutoka nchi zaidi ya 23 tayari wamethibitisha kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka huu, huku waonyeshaji wa ndani zaidi ya 3,772 nao wakithibitisha ushiriki wao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Latifa Mohamed Khamis, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo.
Khamis amesema kuwa maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuanza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai, sambamba na shughuli mbalimbali za maadhimisho maalumu.
Ameeleza kuwa maonesho ya mwaka huu ni ya 50 tangu kuanzishwa kwake, ambapo yataambatana na sherehe za Jubilei ya Dhahabu (Golden Jubilee), ikiwemo hafla maalumu ya usiku wa maadhimisho hayo.

Aidha, amesema maonesho ya biashara ya mwaka huu ni fahari kwa Tanzania, jambo linaloakisiwa na kaulimbiu ya mwaka huu inayolenga kuonesha mchango wa maonesho hayo katika kukuza biashara na uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa TANTRADE, maonesho hayo yamelenga kuimarisha biashara ya kimataifa, huku matumizi ya teknolojia ya kidijitali yakipewa kipaumbele katika kutangaza fursa za biashara na uwekezaji nchini.
Pia kutakuwa na usiku maalumu wa utoaji wa tuzo mbalimbali kwa wadau na wafanyabiashara walioonesha mchango mkubwa katika maendeleo ya biashara nchini.




