Rais wa Kenya, William Ruto, amehimiza kuwapo kwa mshikamano mkubwa wa kikanda kati ya Tanzania na Kenya, huku akiwataja maaduia wakubwa wa nchi hizo ni umasikini na ukosefu wa ajira.
Amesema tofauti kubwa za nchi hizo mbili si tofauti za kisiasa au za kitaifa, bali ni matatizo ya kijamii na kiuchumi.
Akihutubia Bungeni leo Aprili 5, 2026 jijini Dodoma, Rais Ruto amesema kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wanapaswa kuhamisha mtazamo kutoka kwenye mgawanyiko na kuelekeza nguvu katika kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira na umasikini.
“Tunao maadui wengi, lakini maadui wetu si Watanzania wala Wakenya. Maadui wetu ni ukosefu wa ajira na umasikini. Kenya na Tanzania zinategemeana,” amesema Ruto katika hotuba iliyopokelewa kwa makofi na wabunge.
Kiongozi huyo wa Kenya amesisitiza kwamba ustawi wa Taifa moja katika eneo hili umefungamana kwa karibu na mafanikio ya majirani zake, akibainisha kuwa ushirikiano wa kiuchumi ndio msingi wa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki.




