Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea, Noel Kaganda, amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Kimataifa ya Visiwa ya Yeosu, Jong Ki Kim, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo hayo yalijikita katika maandalizi ya Maonesho ya Kimataifa ya Visiwa Duniani 2026 (World Island Exhibition 2026) pamoja na fursa za kupanua ushirikiano kati ya Tanzania, hususan Zanzibar, na Jimbo la Jeollanam katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na ufugaji wa samaki na viumbe maji (aquaculture), kilimo cha kisasa (smart agriculture), biashara, uwekezaji, elimu na ubadilishanaji wa utamaduni.

Katika maonesho hayo yatakayofanyika kuanzia Septemba 5 hadi Novemba 4, 2026, Tanzania kupitia Zanzibar inatarajiwa kupata jukwaa la kutangaza vivutio vyake vya utalii, urithi wa kitamaduni, fursa za biashara na uwezo mkubwa wa uwekezaji kwa washiriki na wadau kutoka mataifa mbalimbali.
Pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kukuza maendeleo endelevu, ubunifu na kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu, huku zikieleza dhamira ya kuendelea kushirikiana katika miradi yenye manufaa kwa pande zote siku zijazo.





