HomeBiasharaWRRB yaanzisha mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa Sekta ya Mifugo

WRRB yaanzisha mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa Sekta ya Mifugo

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika sekta ya mifugo yataimarisha masoko, kuongeza ushindani wa bei na kuwainua wafugaji kiuchumi kupitia upatikanaji wa huduma za kifedha.

Akizungumza Juni 19, 2026, katika Maonesho ya Mifugo na Mnada wa Kimataifa yanayofanyika katika Shamba la Mbogo, Chalinze mkoani Pwani, Afisa Ubora wa WRRB, Anatolius Kabyemera, amesema bodi hiyo imeanza kutekeleza mfumo huo ili kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao kupitia utaratibu rasmi wenye manufaa zaidi.

Kabyemera amesema mfumo huo utaruhusu mifugo kuhifadhiwa katika maeneo maalumu yaliyosajiliwa kama maghala ya mifugo yenye huduma muhimu ikiwemo maji, malisho na wataalamu wa mifugo, wakati ikisubiri kuuzwa kwenye mnada.

“Mfugaji atakapowasilisha mifugo yake katika ghala hilo, atapatiwa stakabadhi ambayo ataweza kuitumia kupata mkopo kutoka taasisi za fedha ambazo tayari tumeshafanya nazo makubaliano, ikiwemo Benki ya NBC,” amesema Kabyemera.

Ameeleza kuwa hatua hiyo itawasaidia wafugaji kuendelea na shughuli nyingine za uzalishaji bila kulazimika kuuza mifugo yao kwa haraka kutokana na mahitaji ya kifedha, hivyo kuongeza thamani ya mifugo na kipato chao.

Kwa upande wake, mfugaji Moringe Gasper, aliyefika kutembelea banda la WRRB katika maonesho hayo, amepongeza mpango huo akisema utaleta mapinduzi katika sekta ya mifugo kwa kuwapa wafugaji fursa sawa na zile wanazonufaika nazo wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.

Amesema wafugaji wengi wana hamu ya kuona mfumo huo unaanza kutekelezwa kwa vitendo ili waweze kupata masoko bora, huduma za mikopo na kuongeza tija katika shughuli zao za ufugaji.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments