Serikali imeanza rasmi hatua za utekelezaji wa Bajeti yenye Mrengo wa Kijinsia (Gender Responsive Budgeting-GRB) kwa kuandaa Tamko la Bajeti yenye Mrengo wa Kijinsia kwa mwaka wa fedha 2026/27, hatua inayolenga kuhakikisha mipango na matumizi ya rasilimali za umma yanazingatia mahitaji ya wanawake, wanaume, wasichana, wavulana na watu wenye mahitaji maalumu ili kukuza maendeleo jumuishi na yenye usawa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akifungua mafunzo kwa Wabunge wa Umoja wa Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (TWPG) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, huku akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imejizatiti kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia mifumo ya upangaji na utekelezaji wa bajeti.


Balozi Omar, alisema Bajeti yenye Mrengo wa Kijinsia si bajeti maalum kwa wanawake, bali ni mfumo unaochambua namna mapato na matumizi ya fedha za umma yanavyowaathiri wanawake na wanaume kwa namna tofauti ili kuhakikisha ugawaji wa rasilimali unazingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii, ikiwemo wanawake, wanaume, wasichana, wavulana na watu wenye mahitaji maalumu.
“Utekelezaji wa bajeti ya namna hii, una mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuondoa vikwazo vya kijinsia vinavyozuia ushiriki kamili wa wananchi katika shughuli za maendeleo, na tafiti zinazoonesha kuwa kufikiwa kwa usawa wa kijinsia kunaweza kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kiwango kikubwa na kuboresha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla” alisema Balozi Omar
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo katika kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia mifumo ya mipango na bajeti, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023.



“Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Serikali tunaanza utekelezaji wa majaribio wa Tamko la Bajeti yenye Mrengo wa Kijinsia katika wizara tisa ambazo ni Kilimo; Elimu, Sayansi na Teknolojia; Katiba na Sheria; Maji; Afya; Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Mifugo na Uvuvi; Viwanda na Biashara; pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo Utekelezaji huu pia unahusisha Ofisi za Wakuu wa Mikoa ya Geita na Singida pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze” aliongeza Balozi Omar
Aliwahimiza wabunge kutumia mafunzo hayo kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya Tamko la Bajeti yenye Mrengo wa Kijinsia ili kuimarisha usimamizi wa bajeti, kutunga sheria na kuishauri Serikali katika kuhakikisha mipango ya maendeleo inawanufaisha wananchi wote kwa usawa.
Alisisitiza kuwa wabunge ni wadau muhimu katika mchakato wa bajeti na kwamba maarifa watakayopata yataimarisha uwezo wa Bunge kusimamia matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana nchini yanakuwa jumuishi na yenye kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi.






