HomeBiasharaPuma Energy Tanzania yatunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Bora 

Puma Energy Tanzania yatunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Bora 

– Ni katika kipengele cha Muagizaji Bora wa Mizigo ya vimiminika (Best Wet Cargo Importer).

– Yatambuliwa kama kampuni bora iliyoonyesha ufanisi, uwajibikaji na mlipa kodi mkubwa nchini Tanzania kwa mwaka 2024/2025.

Dar es Salaam, Julai 1, 2026: Kampuni ya Puma Energy Tanzania imetwaa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Bora katika kipengele cha Mwagizaji Bora wa Mizigo ya vimiminika (Best Wet Cargo Importer), katika hafla ya Tuzo za Rais kwa Walipa Kodi Bora iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Tuzo hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa walipa kodi bora wa mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika hafla iliyowakutanisha walipa kodi bora kutoka mikoa yote 35 ya Tanzania kwa lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi na kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa ambapo tuzo ya Kampuni ya nishati ya Puma Energy Tanzania ilikabidhiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa miaka mingi sasa, Kampuni ya nishati ya Puma Energy Tanzania imeendelea kutoa mchango wake katika maendeleo ya nchi kupitia ulipaji wa kodi, utoaji wa gawio kwa Serikali kama mbia, pamoja na uwekezaji unaolenga kuhakikisha huduma za nishati zinapatikana kwa uhakika, usalama na ufanisi zaidi kwa wananchi na sekta za uzalishaji.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya nishati ya Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah, alisema kampuni inajivunia kupokea tuzo hiyo kwani ni uthibitisho wa misingi imara ya uwajibikaji, uadilifu na uzingatiaji wa sheria ambazo zimeendelea kuwa msingi wa shughuli zake nchini. 

“Tuzo hii ni heshima kubwa kwetu na inatupa nguvu ya kuendelea kutekeleza wajibu wetu kwa ufanisi. Ni matokeo ya jitihada za pamoja za wafanyakazi wetu, ushirikiano wetu mzuri na Serikali pamoja na dhamira yetu ya kuendesha biashara kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria za nchi. Tunaamini kuwa ulipaji wa kodi ni mchango muhimu katika kujenga uchumi imara na kuboresha huduma za kijamii kwa Watanzania,” alisema Bi. Fatma Abdallah

“Tuzo hii inatupa motisha ya kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza mapato ya ndani kupitia ulipaji wa kodi kwa wakati, uwekezaji endelevu na upanuzi wa huduma za nishati zinazochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta mbalimbali za uzalishaji,” aliongeza Bi. Fatma Abdallah

Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kampuni ya nishati ya Puma Energy Tanzania imeendelea kuweka rekodi ya kipekee katika ulipaji wa kodi kwa kuchangia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali kwa Serikali. Kutokana na mchango huo, kampuni imeendelea kutambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utii wake wa sheria za kodi na mchango wake mkubwa katika kuongeza mapato ya Serikali. Tuzo hizi zinadhihirisha dhamira ya dhati ya kampuni hii ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa, kuimarisha utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari, na kuwa mshirika wa kuaminika wa Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Taifa.

Hadi sasa, kampuni hii inaendesha mtandao wa zaidi ya vituo 100 vya huduma za mafuta, kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta pamoja na maghala kadhaa yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini. Kampuni pia inasambaza mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege vinane, ikiwemo viwanja vyote vya kimataifa nchini, na inaendelea kuongoza juhudi za mpito wa matumizi ya nishati safi kupitia Kituo Kikuu cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG Mother Station) kikubwa zaidi barani Afrika pamoja na mtandao unaoendelea kukua wa vituo vya CNG jijini Dar es Salaam na Morogoro.

Aidha, kampuni inaendelea kupanua upatikanaji wa suluhisho za nishati safi za kupikia kupitia Puma Gas, huku biashara yake ya vilainishi (lubricants) na maduka ya Shop Express ikiendelea kuwapatia wateja bidhaa na huduma mbalimbali zenye viwango vya juu vya ubora, sambamba na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments