Serikali ya Marekani imewawekea vikwazo Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Tomoko Akane na wakili mwandamizi wa taasisi hiyo, Abdoulaye Seye, katika hatua mpya ya kuongeza shinikizo dhidi ya mahakama hiyo.
Uamuzi huo umetangazwa jana Jumanne Agosti 18,2026 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio akisema maofisa hao waandamizi wamehusika moja kwa moja katika juhudi za ICC kuchunguza, kuwakamata au kuwafungulia mashtaka viongozi wa nchi ambazo hazijakubali mamlaka ya hiyo, ikiwemo Taifa la Marekani.
Vikwazo dhidi ya Akane na Seye vinawazuia kuingia Marekani kufanya shughuli zao za kifedha kupitia mfumo wa nchi, huku mali zao zilizo ndani ya mamlaka ya nchi hiyo zikifungiwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Marekani zinaeleza kuwa ICC imevuka mipaka yake na kutishia mamlaka ya nchi hiyo, hasa kupitia uchunguzi unaowahusu maofisa wa taifa hilo na Israel.
Marekani si mwanachama wa ICC na haijawahi kuridhia Mkataba wa Roma ulioanzisha mhimili huo, hivyo imekuwa ikipinga mamlaka ya ICC kuwachunguza na kuwafungulia mashtaka raia wake.




