HomeHabariWaterAid, Farm Africa kuunganisha WASH na Kilimo Vijijini

WaterAid, Farm Africa kuunganisha WASH na Kilimo Vijijini

Shirika la WaterAid Tanzania (WAT) na Farm Africa wameingia katika ushirikiano wa kimkakati unaolenga kukabiliana na uhusiano kati ya ukosefu wa huduma bora za maji na usafi, utapiamlo pamoja na kupungua kwa uzalishaji wa kilimo katika maeneo ya vijijini nchini.

Taasisi hizo zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) jana kwa ajili ya kuunganisha huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi wa mwili (WASH) na mipango ya kilimo endelevu pamoja na ustawi wa jamii.

Ushirikiano huo unatambua upatikanaji wa maji salama na usafi wa mazingira kuwa msingi muhimu wa kujenga jamii za wakulima zenye tija na ustahimilivu, hasa wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa kaya za vijijini.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema ushirikiano huo utaunganisha utaalamu wa shirika hilo katika sekta ya WASH na uzoefu wa muda mrefu wa Farm Africa katika mbinu za kilimo endelevu.

Amesema maji yanahusisha kwa karibu afya, utu, usalama wa chakula na maisha ya kila siku ya wananchi, hivyo ushirikiano huo utasaidia kubuni suluhisho endelevu kwa jamii zilizoathiriwa zaidi na ukosefu wa huduma hizo muhimu.

Mzinga amesema makubaliano hayo yanaakisi dhamira ya pamoja ya kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ili ziweze kujiendeleza kwa tija na kujitegemea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Farm Africa Tanzania, Dk. David Ojwang, amesema usafi wa mazingira na usafi wa mwili ni nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe bora.

“Usafi ulioboreshwa ni msingi wa kuimarisha usalama wa chakula na lishe bora nchini,” amesema Dk. Ojwang.

Amesema upatikanaji wa maji si suala la sekta ya afya pekee, bali ni kiungo muhimu kwa wakulima wadogo wanaojitahidi kuzalisha chakula katika mazingira yanayokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema ushirikiano huo unatarajiwa kujikita katika kuandaa mipango ya pamoja, kutafuta rasilimali na kutekeleza miradi katika maeneo ambayo huduma za WASH ni kiungo muhimu cha kuboresha maisha ya wananchi.

Dk. Ojwang amesema kuunganisha huduma za usafi na mbinu bora za kilimo kutasaidia jamii nyingi kujenga maisha yenye uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2030.

Ushirikiano huo unakutanisha uzoefu wa miaka 43 wa WaterAid nchini Tanzania na miaka 35 ya Farm Africa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo vijijini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tangu mwaka 1983 WaterAid imewafikia watu milioni 1.9 kwa huduma za maji na watu milioni 4.3 kwa huduma za usafi.

Mashirika hayo pia yanapanga kuimarisha uongozi wa jamii katika utunzaji wa maliasili, kuboresha upatikanaji wa masoko yenye tija kwa wakulima na kushirikiana kwa maarifa na wadau wengine wa maendeleo katika juhudi za kupunguza umaskini nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments