HomeHabariWakili Nkuba awataka wananchi kuipa ushirikiano Tume ya Jaji Lila

Wakili Nkuba awataka wananchi kuipa ushirikiano Tume ya Jaji Lila


Wakili Msomi Sweetbert Nkuba kutoka Kampuni ya Sweet and Conrad amesema Tume ya Uchunguzi wa Kijinai ya Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, inayoongozwa na Jaji Mstaafu Shabani Ally Lila, imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tanzania.

Amesema wananchi na wadau wote wanapaswa kuipa ushirikiano Tume hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Wakili Nkuba ameyasema hayo leo Agosti 11, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhalali wa Tume hiyo na tofauti zake na Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande.

Kwa mujibu wa Wakili Nkuba, mamlaka ya Rais ya kuunda Tume za Uchunguzi inatokana na Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Uchunguzi, Sura ya 32 ya Sheria za Tanzania.

Amesema mamlaka hayo yanamwezesha Rais kuanzisha Tume ya Uchunguzi pale anapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo, kwa kuzingatia masharti ya Katiba na sheria zinazohusika.

“Kwa hiyo, Tume hii mpya ya Uchunguzi wa Kijinai au Tume ya Jaji Shabani Lila, uhalali wake kama ilivyokuwa Tume ya Jaji Chande unatokana na sheria zetu, kwa maana ya Katiba na Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32,” amesema.

Ameongeza kuwa suala la uhalali wa Tume hiyo halipaswi kuwa na mjadala mkubwa kwa kuwa msingi wake umejengwa katika mamlaka ya kikatiba na kisheria aliyopewa Rais.

Wakili Nkuba pia amezungumzia sifa na uadilifu wa wajumbe walioteuliwa katika Tume hiyo, akisema sehemu kubwa yao ni majaji wenye uzoefu mkubwa katika utoaji wa haki.

Amesema uwepo wa majaji kutoka Mahakama ya Rufani unaongeza imani kwamba Tume hiyo inaweza kutekeleza majukumu yake kwa weledi, usawa na haki, kwa kuzingatia uzoefu wao katika kushughulikia masuala ya kisheria.

Aidha, amesema uamuzi wa kuwahusisha majaji kutoka mataifa mengine, yakiwemo Uganda na Namibia, unaendana na misingi ya sheria inayozingatia umuhimu wa kutokuwa mwamuzi katika jambo ambalo linaweza kuathiri uamuzi wake.

Wakili Nkuba ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kushirikiana na Tume hiyo kwa kutoa taarifa na ushahidi unaoweza kusaidia katika mchakato wa uchunguzi, ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments