Dar es Salaam. Tanzania haiwezi kupata suluhisho la changamoto zake kubwa bila wananchi kuanza kuaminiana, kuvumiliana na kusikilizana, amesema mwanasiasa mkongwe Joseph Warioba Butiku.
Mzee Butiku, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, amesema kuaminiana ni msingi wa demokrasia na ni muhimu katika kusaidia nchi kuvuka changamoto za kisiasa.
“Demokrasia ni imani. Msipoaminiana haitakuwepo hata siku moja,” amesema.
Amesema Watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kuzungumza kwa uhuru lakini kwa heshima, akiwataka wananchi kutambua kuwa kuheshimiana hakumaanishi kumheshimu Rais pekee, bali ni kuheshimiana wao kwa wao.
“Tuanzie kuaminiana,” amesema.
Mzee Butiku amesema suala hilo ni muhimu hasa wakati Tanzania ikiendelea kutafuta majibu kuhusu vurugu zilizohusishwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Amesema tume mpya ya uchunguzi inapaswa kupewa nafasi ya kutafuta ukweli kuhusu kilichotokea na kubaini nani alikuwa nyuma ya vurugu hizo.
“Vurugu hii nani alikuwa nyuma yake? Ni jambo muhimu sana kugfahamu hilo, bila tume unajuaje? Rais anajuaje? Mimi na wewe tunajuaje?” amesema.
Amesema badala ya kuendelea kubishana kuhusu tume hiyo, Watanzania wanapaswa kuiacha ifanye kazi na kusubiri matokeo yake.
“Mimi bado nashauri kama nilivyoshauri ile tume ya kwanza tuikubali. Ameshafanya, tuache maneno mengi, ifanye kazi tuje tuone matokeo ya kazi yake,” amesema.
Kwa mujibu wa Mzee Butiku, taarifa zitakazopatikana zinaweza kusaidia Rais kupata ushauri na hatimaye kusaidia taifa kuelewa kilichotokea na namna ya kwenda mbele.
Amesema vijana nao wanapaswa kupewa nafasi ya kuzungumza na viongozi wao na kusikilizwa, lakini mawasiliano hayo yanapaswa kufanyika kwa heshima.
“Nyinyi vijana, mwamini Rais wenu,” amesema.
Amesema mfumo wa vyama vingi nao unahitaji kuvumiliana, akisema upinzani una wajibu wa kuikosoa Serikali lakini unapaswa kufanya hivyo kwa heshima, kuaminiana na ukweli.
“Upinzani huu usimame kwenye heshima na kuaminiana na kiwango fulani cha ukweli,” amesema.
Amesema Tanzania haiwezi kufikia suluhisho ikiwa kila upande utapinga kila jambo, akisisitiza umuhimu wa kujenga hoja badala ya makabiliano.
“Tusipingane kila kitu, tuanze kuongozana kwa hoja,” amesema.
Mzee Butiku amesema Watanzania wanapaswa pia kutambua kuwa nchi ina Rais mmoja na kumpa nafasi ya kuongoza huku wananchi wakiendelea kushiriki katika kutatua changamoto zilizopo.
“Tunaye rais mmoja. Narudia tunaye rais mmoja. Kila mtu hawezi akageuka akawa rais,” amesema.
Amesema kujenga upya uaminifu miongoni mwa Watanzania ni muhimu kama nchi inataka kupata njia ya kwenda mbele baada ya mvutano unaohusishwa na uchaguzi huo.




