HomeBiasharaMwenge wazindua tawi jipya la CRDB Maganzo, Kishapu

Mwenge wazindua tawi jipya la CRDB Maganzo, Kishapu

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amezindua tawi jipya la Benki ya CRDB katika Kata ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, hatua inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mikopo wa CRDB, Exavery Makwi, amesema benki hiyo inaendelea kuimarisha huduma kwa wateja ili kuwawezesha kuongeza kipato na kujenga uchumi endelevu wa familia.

Amesema Tawi la CRDB Maganzo lilianzishwa Septemba 2016 likiwa na watumishi watatu katika ofisi ndogo iliyopo Mtaa wa Oysterbay, lakini limeendelea kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo na Wilaya ya Kishapu kwa ujumla.

“Ndani ya muongo mmoja wa kutoa huduma, tawi letu limekua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi za wananchi wa hapa Maganzo na Wilaya nzima ya Kishapu, ndiyo maana tumelazimika kuwa na ofisi kubwa zaidi na kuhamia hapa Machinjioni,” amesema Makwi.

Amesema CRDB ina zaidi ya matawi 260 nchini, yakiwemo 25 katika Kanda ya Magharibi inayojumuisha Shinyanga, Tabora, Kigoma na Geita, yanayohudumia sekta mbalimbali ikiwemo madini, kilimo, ufugaji na biashara.

Makwi amesema ujenzi wa Tawi la CRDB Maganzo umegharimu Sh700 milioni, huku akiishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha kuendesha shughuli zake na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Uzinduzi wa tawi hilo ni sehemu ya shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazolenga kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusogeza huduma muhimu kwa wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments